Habari

Korti yaagiza Ndiang’ui asikamatwe huku polisi wakilaani vikali ‘mtindo wa watu kujiteka’

Na RICHARD MUNGUTI, JOSEPH WANGUI July 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA kuu Alhamisi iliamuru polisi wasimkamate mtalaam wa masuala ya mawasiliano na gwiji wa matangazo katika mitandao ya kijamii Bw Ndiang’ui Kinyagia aliyejitokeza baada ya kukaa mafichoni kwa siku 13.

Hata hivyo, Jaji Chacha Mwita alisema polisi wako huru kuandikisha taarifa kutoka kwa Bw Kinyagia “mradi ameandamana na mawakili Kibe Mungai na Wahome Thuku.”

Kujitokeza kwa Bw Kinyagia mbele ya Jaji Mwita jana kulimwokoa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohammed Amin pakubwa kwa vile alikuwa amefika kortini kueleza “kule maafisa wa DCI walikompeleka Kinyagia baada ya kumtia nguvuni Juni 21, 2025.”

Bw Amin alikuwa ameagizwa na Jaji Mwita afike kortini Alhamisi mwenyewe kueleza aliko Bw Kinyagia ambaye alitoweka “alipokamatwa na watu walioaminika kuwa maafisa wa DCI.”

Lakini mwendo wa saa tano kasoro dakika 20, Bw Kinyagia alijisalamisha mbele ya Jaji Mwita, akiandamana na wakili Thuku na binamuye Lilian Wanjiku Gitonga.

Mwanablogi huyo aliyeonekana mchovu na kuchanganyikiwa alikaa karibu na mama yake na watu wengine wa familia.

Naye kinara wa DCI, Bw Amin alifika kortini saa tano asubuhi akiandamana Naibu wa Inspekta Jenerali Gilbert Masengeli.

Maafisa wengine zaidi ya 100 wa idara ya DCI wakiwa wameabiri magari aina ya Subaru walifurika kortini kujua hatma ya Bw Amin.

Jaji Mwita alikuwa amemtaka Bw Amin afike kortini kueleza kilichompata Bw Kinyagia aliyeripotiwa kutoweka baada ya maafisa wa DCI kufika nyumbani kwake kumhoji.

Mahakama ilielezwa kwamba maafisa wa DCI walikuwa wanamsaka Bw Kinyagia kwa kusambaza habari za uchochezi Juni 2025 akiwataka wananchi wavamie Ikulu ya Rais Juni 25, 2025 wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja ya kumbukumbu za vijana zaidi ya 60 kuuawa na polisi Juni 25, 2024 na polisi Gen Z walipovamia bunge.

Kabla ya Bw Amin kuingia kizimbani kusimulia anachofahamu kuhusu kutoweka kwa mwanablogi huyo, wakili Mungai alieleza mahakama Bw Kinyagia “tayari amefika kortini na ameketi”.

Jaji alielezwa Bw Kinyagia alimpigia binamuye na kumweleza kwamba yuko salama na alikuwa amejificha polisi wasimtie nguvuni.

Bw Mungai alieleza mahakama Bw Kinyagia anahofia maisha yake na angeliomba mahakama iamuru polisi wasimkamate.

Pia aliomba mahakama iahirishe kesi hiyo kuwezesha familia ya mlalamishi (Kinyagia) kumpeleka hospitali kwa vile sio buheri wa afya.

“Bw Kinyagia kuja mbele,” Jaji Mwita alimwita mlalamishi huyo.

Bw Kinyagia alitoka alipokuwa ameketi na kusimama mbele ya Jaji Mwita.

“Asante nimethibitisha uko hai,”Jaji Mwita alisema kisha akaongeza , “Nakukabidhi Wakenya ukiwa hai. Niliamuru ufikishwe kortini leo aidha ukiwa hai ama maiti yako. Lakini uko hai. Rudi ukae.”

Baada ya Jaji Mwita kusema kwamba maagizo aliyotoa yamefuatwa aliwataka Bw Kinyagia na Bw Amin waliofika kortini waruhusiwe kuendelea na shughuli zao.

Hata hivyo, mawakili Martha Karua, Mungai na rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Faith Odhiambo waliomba Bw Kinyagia apelekwe hospitali.

Pia waliomba wamhoji Kinyagia ndipo awaambie alipokuwa na kilichompata.

Jaji Mwita alimruhusu Bw Amin kurudi kazini baada ya kusema familia ya Bw Kinyagia inahitaji muda kujumuika naye na pia kumpeleka hospitali.

Akaagiza Jaji Mwita “Polisi wameamriwa wasimtie nguvuni Bw Kinyagia. Atajipeleka katika afisi za DCI akiandamana na mawakili wake kuandika taarifa.”

Jaji huyo aliamuru kesi hiyo iendelee Julai 18, 2025.

Mahakama ilielezwa na Bi Karua na mawakili wa LSK kwamba walikuwa wamejiandaa na maswali 50 kumhoji Bw Amin kuhusu utekwaji nyara wa Bw Kinyagia.