Dimba

NOC-K yaamrishwa kuandaa uchaguzi mkuu wiki mbili zijazo

Na CECIL ODONGO July 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BUNGE la Kitaifa jana liliamuru mirengo miwili inayozozania uongozi wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) kuondoa kesi kortini na kuandaa uchaguzi wa kitaifa katika wiki mbili zijazo.

Kamati ya Bunge kuhusu Michezo na Utamaduni inayoongozwa na Mbunge wa Webuye Magharibi, Dan Wanyama, ilisema wanamichezo wameonyeshwa vitimbi, lawama na kesi zisizokwisha, lakini sasa kura ya NoC-k lazima iandaliwe.
Mirengo miwili inayozozania uongozi ni Team New Dawn inayoongozwa na Shadrack Maluki kutoka mchezo wa judo na Team Service Team chini ya Francis Mutuku kutoka mchezo wa tenisi.
“Mnaagizwa muondoe kesi zote mahakamani kisha uchaguzi uandaliwe ndani ya wiki mbili. Kila mtu ambaye yuko kwenye daftari ya Msajili wa Michezo ashiriki bila kutatizwa,” akasema Wanyama ambaye alionyesha wazi jinsi alivyoghadhabishwa na mzozo huo wa uongozi.
Kamati ya Bunge pia iliagiza orodha ya kwanza iliyochapishwa na Msajili wa Michezo ndiyo itumike kwa uchaguzi huo.
Kura ya NoC-K imekuwa imeahirishwa mara mbili kutokana na kesi kortini.
“Nimekuwa michezo kwa miaka mingi na ninajua sarakasi hizi ambazo mnafanya bila kuzingatia kuwa ni wanamichezo ndio wanaumia.
“Msiwashike mateka wanamichezo kwa sababu ya maslahi yenu ya kibinafsi mkisingizia kesi za korti. Acheni kura iandaliwe ili mwaniaji maarufu awahi ushindi,” akaongeza Wanyama.
Wanachama wengine wa kamati waliohudhuria kikao hicho kando na Wanyama ni Mbunge Mwakilishi wa Kakamega, Elsie Muhanda, Charles Ngusya Nguna (Mwingi Magharibi), Letilipa Domnic (Samburu Kaskazini), Paul Ekwom Nabuin (Turkana Kaskazini), Richard Yegon (Bomet Mashariki) na Mbunge Mteule Jackson Kosgei.
Kamati hiyo pia iliamrisha Rais wa sasa wa NoC-K Paul Tergat achukue usukani na kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unaandaliwa kwa njia huru.
Akiongea katika kikao hicho Tergat alisisitiza kuwa uchaguzi ungelikuwa ushamalizika, na kwamba sintofahamu iliyopo inaumiza Kenya na kutatiza maandalizi yake kwa mashindano mbalimbali.
Mzozo kwenye mashirikisho ya handiboli, voliboli, taekwondo na triathlon kuhusu nani anastahili kupiga kura kwenye uchaguzi wa NoC-K ulichangia kura hiyo kukosa kuandaliwa mnamo Aprili 24.
Kulikuwa na mzozo katika mashirikisho hayo manne iwapo katibu au mwenyekiti wa shirikisho ndiye anastahili kupiga kura.
Mnamo Juni 19, Jaji wa Mahakama ya Eldoret Reuben Nyakundi alisimamisha uchaguzi kutokana na kesi iliyowasilishwa na Rais wa Shirikisho la Triathlon Joyceline Nyambura na wengine watatu kuhusu uwazi katika kura.