DCP yamuweka Karish kumenyana na Njagagua wa UDA uchaguzi mdogo Mbeere North
UCHAGUZI mdogo unaokaribia katika eneo bunge la Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu, unatarajiwa kuwa wa kusisimua huku upinzani ukimtangaza mwanamuziki kumenyana na wakili anayepigiwa debe na serikali.
Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge Geoffrey Ruku kuteuliwa Waziri wa Utumishi wa Umma, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa awali na Justin Muturi kabla ya kuondolewa na Rais William Ruto.
Kwa sasa, wawaniaji wakuu katika uchaguzi huu wa ushindani mkali ni msanii maarufu na Mwakilishi Wadi wa Muminji kwa mihula mitatu, Newton Kariuki maarufu kwa jina la kisanii Karish, ambaye ana zaidi ya nyimbo 100.
Karish ameidhinishwa na chama cha Democratic Party (DP), ambacho ni sehemu ya muungano mpya wa upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Democratic Party inaongozwa na Bw Justin Muturi, Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa na Mwanasheria Mkuu wa zamani.
Kwa upande mwingine, wandani wa Rais Ruto wanamuunga mkono Muriuki Njagagua, wakili mkongwe, msemaji mahiri na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Consolidated. Anaonekana kuwa mgombea bora wa kukabiliana na mawimbi ya upinzani yanayopata nguvu katika eneo la Mlima Kenya.
Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Njagagua alishindwa na Bw Ruku kwa tofauti ndogo ya kura 647 pekee.