Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Wanaomkosoa Prof Ngugi wa Thiong'o bado hawajamshiba

February 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA PROF KEN WALIBORA

LIMEFANYIKA kongomano kubwa kuhusu tafsiri katika jiji la Nairobi mnamo Februari 8 na 9 mwaka huu. Mwandishi maarufu Prof Ngugi wa Thiong’o alikuwa miongoni mwa watoaji wa mada katika kongomano hilo.

Ajabu ya dunia ni kwamba watu wanakuwa na maoni tofauti kuhusu aghalabu kila jambo maishani. Sikuwapo wakati wa Prof Ngugi kutoa hotuba yake.

Nilikuwa nimekwenda huko Kuria katika shule ya upili ya Kubweye kuwahamasisha vijana kuhusu umuhimu wa Kiswahili kwa mwaliko wa Mwalimu Zablon Marwa.

Basi rafiki mmoja akaniambia Prof Ngugi aliwasilisha hotuba ndefu sana kuhusu tafsiri na siasa za tafsiri, hotuba ambayo wengi iliwachusha kwa urefu na uchapwa wake. Nilishangaa sana kusikia kauli hiyo.

Namwelewa Prof Ngugi. Nimewahi kuzisikiliza hotuba zake ndani na nje ya nchi hii. Nilimsikiliza mara ya kwanza mwaka 2004 alipokuwa ndio mwanzo anarejea nyumbani kutoka uhamishoni.

Alitoa hotuba ya kusisimua katika ukumbi wa Taifa Hall katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Sikumbuki urefu wala ufupi wa hotuba yake bali mantiki na muwala wake na kina cha fikira.

Niliwahi kumsikiliza huko Marekani na Ujerumani. Tukiwa Ujerumani Mkenya mmoja aliniambia mbona mwandishi huyu ni maarufu ila hotuba yake haina mvuto.

Basi kusikia kwamba hotuba ya Ngugi haina mvuto si jambo ninalolisikia kwa mara ya kwanza. Nimelisikia mara moja moja.

Sijui wakosoaji wake wanataka azungumze vipi? Kwa watu wanaothamini mawazo na utunduizi wa kitaaluma, Prof Ngugi anakidhi haja tena sana. Anachokonoa akili za hadhira yake ya kusema bila kuogopa, kusema lolote na kulisema bila hatihati.

Aidha aghalabu anazamia lulu masuala ya kikoloni na kikoloni-mamboleo katika maandishi na mazungumzo yake kwa namna isiyokuwa na mfano.

Na ingawa sikusikia hotuba yake Dkt Leonard Chacha, ambaye nilikuwa kwao Kuria, alihudhuria kongomano Nairobi naye aliniambia Ngugi alitoa hotuba nzuri sana.

Kinyume na mkosoaji wa hotuba hiyo, Dkt Chacha alinihakikishia kwamba hotuba hiyo ilikuwa na uketo na ukakamavu wa kupigiwa mfano. Mathalan, kaniambia kwamba Ngugi alizungumzia historia nzima ya tafsiri na ushawishi wa kikoloni katika historia hiyo.

Kwa mtu anayepata riziki yake kwa kuajiriwa na vyuo vikuu vya mataifa ya Magharibi, ni ujasiri mkubwa kwake kuendelea kuzikomoa asasi za kidhalimu za kimagharibi.

Kama si mwepesi katika hotuba yake hilo si muhimu. Prof Ngugi ni mmojawapo wa wanafalsafa muhimu katika bara la Afrika.

Si haki kumtazamia awe msemaji hodari PLO Lumumba au asema wanachotaka Wazungu na Weusi waliokumbwa na kasumba ya ukoloni. Wanaomtarajia awe hivyo, wanapitwa na kina cha fikra zake na tija ya hekima yake.

Prof Ngugi ndiye amekuwa mstari wa mbele kuwakumbusha Wakenya na Waafrika kwamba sio kila kitu chao ni kibaya. Anawakumbusha wasichukie lugha zao na majina yao na utamaduni wao. Jamani acheni kumponda mzee wetu.