Habari

Bidhaa ghushi za sigara, dawa, urembo zimeenea Kenya – Ripoti

Na EDNA MWENDA July 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIGARA, dawa za kutibu maambukizi ya bakteria na dawa za kutibu malaria, bidhaa za urembo na ngozi ni miongoni mwa zinazoghushiwa zaidi nchini Kenya.

Kwa mujibu wa ripoti mpya, hali hii inazua wasiwasi kuhusu kupotea kwa mapato na hatari za kiafya na usalama kutokana na bidhaa hizo feki kuenea sokoni.

Ripoti hiyo mpya ilizinduliwa na Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Ghushi (ACA), ikifichua kuenea kwa bidhaa ghushi katika sekta kuu kama vile kilimo, famasia, pombe, vipodozi, na vifaa vya kielektroniki.Sekta ya tumbaku inaongoza sigara, zikichangia asilimia 89.47.

“Dawa za kutibu maambukizi ya bakteria na dawa za malaria zinachangia asilimia 89.28 ya bidhaa feki, jambo ambalo linaweka afya ya umma hatarini kwa kupunguza ufanisi wa matibabu na usalama wa wagonjwa,” ilisema ACA.

Sekta ya kilimo iliathirika kwa asilimia 89.16 huku waliohojiwa wakitaja mbolea na dawa za kuua wadudu kama bidhaa zinazoghushiwa zaidi, zikifuatiwa na vipuri vya magari kwa asilimia 81.89.

Wakenya pia wananunua bidhaa ghushi bila kujua kama vile vipodozi, dawa za meno, karatasi za choo, nepi, shampoo, nywele bandia na bidhaa za nywele ambazo zinachangia asilimia 88.32 ya bidhaa bandia.Asilimia 81.89 ya washiriki walitaja vipuri vya magari ya magurudumu manne kuwa bidhaa ghushi zaidi katika sekta ya magari.

Katika kilimo, zaidi ya nusu ya waliohojiwa walisema mbolea (asilimia 54.29) na chakula cha mifugo (asilimia 45.6) haziidhinishwi ipasavyo.

Utafiti huo ulifanyika mwezi Agosti mwaka jana kwa ushirikiano kati ya ACA na Chuo Kikuu cha KCA, ukihusisha watu 2,185 kutoka kaunti nane zikiwemo Mombasa, Nairobi, Nakuru, Nyeri, Machakos, Kisumu, Garissa, na Busia.Mbegu (asilimia 34.9) na vifaa vya kilimo (asilimia 13.66) pia vimeathiriwa.

“Uwepo wa pembejeo bandia unatishia utoshelevu wa chakula na maisha ya wakulima. Sheria kali zaidi, adhabu kali, na kampeni za uhamasishaji wa umma zinahitajika kupunguza athari za bidhaa feki katika sekta hii muhimu,” ilisema ACA.

Utafiti huo ulifanyika mwezi Agosti mwaka jana kwa ushirikiano kati ya ACA na Chuo Kikuu cha KCA, ukihusisha watu 2,185 kutoka kaunti nane zikiwemo Mombasa, Nairobi, Nakuru, Nyeri, Machakos, Kisumu, Garissa, na Busia.

ACA ilitaja maeneo kadhaa ya kutoa na kuuza bidhaa ghushi ikiwa ni pamoja na Hong Kong (China), Singapore, na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambazo zinahusishwa na biashara ya bidhaa ghushi.

Waliohojiwa walieleza wasiwasi kuhusu usalama wa vinywaji visivyo na kileo kama vile juisi na soda ambazo zilichangia takriban asilimia 75.89 ya bidhaa bandia.