Vigogo wa upinzani wataepuka mkosi?
HUKU ikisalia miezi 25 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, mazungumzo ya kusuka muungano mkubwa wa kisiasa wa vyama vya upinzani yameanza kushika kasi.
Lengo kuu ni kuungana ili kumshinda Rais William Ruto, lakini swali linalozidi kutawala Wakenya wengi ni iwapo, viongozi wa upinzani wataweza kuepuka mkosi wa kugawanyika ambao umevuruga juhudi hizo katika historia ya kisiasa Kenya.
Tayari, zaidi ya viongozi saba mashuhuri wameanza harakati zao binafsi za kuwania urais. Waliotangaza azma zao kwa sasa ni pamoja na Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Eugene Wamalwa, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Fred Matiang’i. Kila mmoja wao anaonekana kujipanga kwa nguvu, akitumia uungwaji mkono wa jamii na eneo analotoka kama mtaji wa kisiasa.
“Tunapinga madai kwamba kuna migawanyiko katika timu yetu. Tuna lengo moja kuu — kuikomboa Kenya kutoka kwa utawala wa sasa — na hatuwezi kusaliti imani ya mamilioni ya Wakenya wanaotutegemea,” Bw Musyoka alisema alipoungana na vigogo wa upinzani kwa mikutano ya hadhara eneo la magharibi.
“.Lengo letu ni kuimarisha uhusiano wetu na kujenga msingi imara wa kushirikiana, Kwa wakati ufaao, tutaafikiana kuhusu atakayekuwa mgombea wetu wa urais,” aliongeza.
Katika mahojiano ya runinga wiki hii, Matiang’i alitangaza azma yake ya kuwania urais, akieleza kuwa tayari anashirikiana na viongozi wa upinzani na pia anawasiliana na wananchi kuhusu changamoto zinazokumba taifa.
“Kenya inahitaji kiongozi wa kweli, mwaminifu na mwenye uwezo wa kujenga maridhiano,” alisema.
Hata hivyo, changamoto kubwa kwa upinzani sio uhaba wa wagombeaji urais bali kukosekana kwa umoja wa kweli. Historia ya siasa za Kenya imejaa mifano ya mikataba ya kisiasa inayotumbukia nyongo, usaliti wa dakika ya mwisho, na makundi yanayovutana chini kwa chini.
Mfano wa wazi ni mkataba wa 2013 kati ya Uhuru Kenyatta na Musalia Mudavadi. Ingawa walifikia makubaliano ya kumuunga mkono Mudavadi kuwa mgombea wa urais kupitia chama cha UDF, makubaliano hayo yalivunjwa muda mfupi baadaye baada ya Uhuru kusema alisukumwa na “nguvu za giza.”
Kabla ya uchaguzi wa 2022, muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ulioundwa na Kalonzo, Mudavadi, Wetang’ula na Gideon Moi ulishindwa kuafikiana kuhusu mgombea mmoja.
Mivutano hiyo ilisababisha Mudavadi na Wetang’ula kutangaza kushirikiana na William Ruto, katika kile Mudavadi aliitwa “tetemeko la ardhi la kisiasa.” Hatimaye, wawili hao walivuna matunda ya uamuzi huo kwa kupata nyadhifa za juu serikalini.
Gavana Amason Kingi pia alionekana kwa ghafla wakati wa mikutano ya awali ya OKA, na baadaye alijiunga na upande wa Kenya Kwanza. Hii ni ishara nyingine ya jinsi hali ya kisiasa ilivyo dhaifu na isiyotabirika.
Wachambuzi wa siasa wanasema huku vinara wa upinzani wakiahidi kuwa safari hii watasimamisha mgombea mmoja, ishara za ndani zinaonyesha kuwa hali bado ni tete. Viongozi kama Kalonzo na Gachagua wameonekana kuendesha mikutano kwa pamoja, lakini kuna wasiwasi kuhusu iwapo wataungana hadi mwisho.
Chama cha Jubilee kinasemekana kumwamini Matiang’i kuwa mgombea urais kumenyana na Rais William Ruto.
“Mara nyingi, huwa kuna fuko wa chama au muungano tawala katika siku za awali za kusuka muungano wa upinzani. Vinara wa upinzani huwa wanakosa kutambua mapema na kupata pigo akifichua mikakati yao kwa upande unaotetea mamlaka uchaguzini,” asema mchanganuzi wa siasa Musa Koli.
Anasema sio ajabu mmoja au watu wa vinara wa upinzani akawa ajenti wa serikali ambaye atasababisha juhudi zao zigonge mwamba.
Kuna pia wanaolenga biashara na ndio huwa wananunuliwa na chama tawala na hivyo kusambaratisha upinzani wakiondoka.
“Changamoto kubwa kwa upinzani Kenya huwa sio uchaguzi wenyewe, bali kukosekana kwa umoja wa kimkakati. Katika uchaguzi wa 1992 na 1997, upinzani ulikuwa na jumla ya zaidi ya asilimia 50 ya kura, lakini bado Rais Moi alishinda kwa wingi wa kura. Hali kama hiyo inaweza kujirudia iwapo upinzani utasambarika,” asema na kuongeza kuwa Moi alikuwa akihakikisha wapinzani wake waligawanyika.
Ili upinzani uweze kuwa na muungano thabiti ni lazima uwe na msingi imara – vyama vilivyo na miundo madhubuti na maelewano ya kisheria. Bila misingi hiyo, mikataba yoyote huwa ni ya muda mfupi na inavunjwa kwa urahisi.
“Wanasiasa wa Kenya wamezoea kubadilisha msimamo hima kwa kununuliwa na wanaotetea mamlaka.Huku upinzani ukiwa katika harakati za kutafuta mgombea mmoja, historia ya usaliti, ubinafsi, na kushindwa kuaminiana inaelekea kujirudia. Wapiga kura, hasa vijana, wanaendelea kuangalia kwa makini kama viongozi hawa wataweza kujifunza kutoka kwa makosa ya nyuma,” asema.
Ruto alitumia hali hiyo ya sintofahamu kwa faida yake kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 akikejeli OKA kwa “kukosa mgombea na ajenda.” Hali ilivyozidi kuwa ya sintofahamu, Uhuru aliwaita viongozi wa upinzani Ikulu ya Mombasa na kuripotiwa kuwaomba wamuunge mkono Raila.