Habari

THOMAS CHERUIYOT: Ipo haja kukumbatia matumizi ya Kiswahili nje ya mipaka ya darasa

Na THOMAS CHERUIYOT July 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LUGHA ni chombo kikuu cha binadamu cha kueleza maana – kwa maneno au bila maneno.

Inatumika kwa malengo mengi: kujenga madaraja, kuunganisha jamii, kuhimiza amani, kueneza furaha na kukuza upendo.

Hata hivyo, lugha pia inaweza kugawanya, kuchochea chuki na hata kuhalalisha vurugu ikiwa itatumiwa vibaya. Kwa kuwa ni chombo chenye nguvu, matumizi ya lugha yanahitaji uangalifu na uwajibikaji mkubwa.

Kiswahili, kama lugha ya mawasiliano ya pamoja, kina uwezo wa kipekee wa kuwaleta watu pamoja kutoka makundi tofauti ya kikabila, kidini, kiumri na kijamii. Ni tanuri linaloyeyusha tamaduni mbalimbali na kutumika kama nyenzo ya kuleta usawa, kwa kuunganisha jamii licha ya tofauti zao.

Tangu kizaliwe Afrika Mashariki, Kiswahili kimevuka mipaka ya kieneo na kufika mataifa ya mbali kama Japan, Amerika na Finland.

Leo hii, kinazungumzwa na watu zaidi ya milioni 250 duniani kote na kinawakilisha ishara ya mshikamano na utambulisho wa kina. Katika takriban nchi 15 za Afrika, Kiswahili ni lugha kuu ya biashara na mawasiliano.

Umuhimu wake wa kimataifa ulithibitishwa na UNESCO iliyotangaza tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU), ikitambua Kiswahili kama nyenzo muhimu ya kukuza mazungumzo ya kitamaduni na utofauti.

Mwaka huu, chini ya kauli mbiu “Kiswahili kwa Umoja, Amani, na Ustawi,” Chuo Kikuu cha Eldoret kitaadhimisha leo nafasi ya Kiswahili katika kuendeleza amani, mshikamano na mazungumzo ya kitamaduni.

Tukio hilo linatufundisha kuwa Kiswahili si lugha tu, bali ni chombo cha amani, maendeleo na ustawi endelevu. Chuo Kikuu cha Eldoret kitaungana leo na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Kiswahili.

Tunasihi wote kukumbatia Kiswahili katika ngazi zote – kujifunza shuleni, kukitumia nyumbani, kukitumia katika biashara na kukijumuisha katika taasisi. Wito wetu mkubwa ni kutumia Kiswahili kukuza ujumuishaji wa kijamii na kupunguza migogoro.

Kupitia Idara yake ya Lugha na Fasihi, Chuo Kikuu cha Eldoret kimejikita katika kukuza Kiswahili. Chuo kimezalisha wahitimu wengi wa Kiswahili wanaohudumu katika sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Hivi majuzi, chuo kilizindua Taasisi ya Kiafrika ya Masomo ya Maendeleo, taasisi ya umahiri inayolenga lugha za asili za Kiafrika, ambapo Kiswahili kina nafasi ya kipekee.

Hapa, Kiswahili si somo tu – ni njia ya kubadilishana maarifa, kukuza maelewano ya kitamaduni, na kuimarisha amani na ustawi.

Mwandishi ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Eldoret