CHRIS ADUNGO: Wapenzi wa lugha watazamia SIKIDU iwatunuku Baraza la Kiswahili
WAPENZI wa Kiswahili humu nchini wamedhamiria kutumia maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU) mwaka huu kushinikiza Serikali ya Kenya kuharakisha mchakato wa kuunda Baraza la Kiswahili.
Azma ya kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya (BAKIZE) ilianza katika miaka ya 1980.
Hata hivyo, ukosefu wa utashi wa kisiasa kuhusu mchakato huo umeonekana kuponza ndoto hiyo nzima mpaka sasa, kiasi kwamba urasmi wa Kiswahili nchini Kenya umesalia tu kuwa sehemu ya maandishi ndani ya Katiba.
Nchi ya Tanzania kwa mfano, ina Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) lililoundwa 1967. Baraza hilo linaratibu, kusimamia asasi na mawakala wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia linahimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida na kushirikiana na mamlaka mbalimbali zinazohusika kuthibitisha tafsiri sanifu za istilahi.
Majukumu mengine ni pamoja na kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa serikali na taasisi nyingine, kuchapisha jarida au toleo linalohusu lugha na fasihi ya Kiswahili na kushirikiana na mashirika ya kitaifa pamoja na watu binafsi kufuatilia, kushauri na kusimamia shughuli zinazolenga kukuza Kiswahili kitaifa na kimataifa.
Isitoshe, hutoa ushauri kwa waandishi na wachapishaji watumie Kiswahili fasaha na kushirikiana na Wizara ya Elimu.