Raila: Murkomen aliniomba msamaha baada ya amri yake kwamba polisi waue raia
WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga sasa anadai kuwa Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen alimwomba msamaha, na Wakenya, kufuatia amri lake kwamba polisi wawapige risasi “raia watakaokaribia vituo vya polisi.”
Akijibu maswali kutoka kwa wanahabari Jumatatu, Julai 7, 2025, baada ya kuwahutubia katika mkahawa wa Serena, Nairobi, Bw Odinga aliongeza kuwa Waziri huyo alimwahidi kuwa polisi sasa watakoma kuwatendea raia ukatili.
“Nilisema agizo kama hilo haikubaliki na aliniomba msahama pamoja na wananchi. Polisi wanafaa kuwa waangalifu wanapoitwa kudumisha amani. Hii ndio maana napendekeza mageuzi yatakayowezesha kikosi cha polisi kuwa watumishi kamili wa wote wala sio wakatili,” akasema akijibu swali kutoka kwa mwanahabari Seth Olale aliyesaka maoni yake kuhusu agizo hilo lililoibua kero kubwa nchini.
Hata hivyo, Bw Odinga hakufafanua namna ambayo Bw Murkomen aliomba msamaha huo kwani hajawahi kufanya hivyo kupitia taarifa rasmi au kupitia majukwaa ya hadhara.
Kile Waziri huyo amefanya ni kujitetea kwamba alinukuliwa nje ya muktadha ambamo aliitolea amri hiyo, akiwa eneo la Kikuyu kukagua uharibifu uliosababishwa na wahuni walioteketeza kituo cha polisi cha Kikuyu wakati wa maandamano ya Juni 25.
Jumatatu, Bw Odinga alisema japo fujo na uharibifu wa mali ulioshuhudiwa wakati wa maandamano hayo, polisi hawafai kutumia mbinu zisizokubalika kikatiba kudhibiti maovu hayo.
“Tulishuhudia umwagikaji mkubwa wa damu juzi. Baadhi ya watoto waliojitokeza kushiriki maandamano waliuawa— wengi na polisi,” akasema.
“Polisi hawafai kuwauwa watu kwa risasi. Hawana kibali cha kutoa uhai wa mwanadamu. Endapo mtu ametenda uhalifu, kamata mtu kama huyo na kuwasilisha mbele ya mahakama,” akaongeza Bw Odinga.
Kwa hivyo, kwenye ujumbe wake kwa taifa kuhusu Siku ya Saba Saba, kiongozi huyo wa ODM alipendekeza Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ifanyiwe mageuzi ili kuimarisha mahusiano kati ya maafisa wake na raia.
“Sharti huduma ya polisi ifanyiwe mageuzi ili iwe mtetezi wa watu, mtumishi,” Bw Odinga akaeleza.
Aidha, alipendekeza kubuniwa kongamano la kitaifa linashirikisha watu wa vizazi vyote kushughulikia masuala ya uwazi, uwajibikaji, ufisadi na mienendo ya kudharua sheria miongoni mwa watumishi wa umma nchini.
Hayo ni miongoni mwa masuala ambayo vijana wa Gen Z wamekuwa wakiitaka serikali ishughulikie.