Habari

Idadi ya waliokufa kwenye maandamano ya Saba Saba yapanda hadi 31 — KNCHR

Na CHARLES WASONGA July 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

IDADI ya watu waliouawa wakati wa makabiliano kati ya walinda usalama na waandamanaji wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saba Saba, Jumatatu sasa imepanda hadi 31.

Kulingana na takwimu za hivi punde kabisa zilizotolewa na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR) watu 107 wamethibitishwa kujeruhiwa, watu wawili kutekwa nyara na wengine 532 kukamatwa na polisi katika kaunti 17 zilizoshuhudia maandamano siku hiyo Julai 7, 2025.

Maandamano yaliyoongozwa na vijana wa Gen Z kwa mara nyingine yalitekwa na wahuni waliotumia nafasi hiyo kuwavamia watu na kuwaibia, kupora na kuharibu mali ya thamani ya mabilioni ya pesa.

“Tume ya KNCHR inalaani vikali vitendo vyote vya ukiukaji wa Haki za Kibinadamu na kuhimiza uwajibikaji kwa wahusika wote-wakiwemo polisi, raia na wadau wote. Kwa mara nyingine tunatuma rambirambi kwa wale waliopoteza wapendwa wao na kuwatakia afueni ya haraka wale waliojeruhiwa,” ikasema kwenye taarifa iliyotiwa saini na naibu mwenyekiti Dkt Raymond Nyeris.

Aidha, tume hiyo ililaani mtindo wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi na risasi wanapopambana na waandamani ikikariri kuwa “ni wajibu wa polisi kulinda maisha na mali.”

Wakati huo huo, Jumanne familia zilizopoteza wapendwa ziliendelea kuwataka polisi wakome kuwaua watu kiholela nyakati za maandamano.

Nao wafanyabiashara walilalamikia hasara waliyopata baada ya wahuni kupora mali zao.

Kwa upande wao wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua waliisuta serikali kwa kushindwa kudumisha usalama nyakati za maandamano.