Korti yazima polisi kufunga jiji wakati wa maandamano
MAHAKAMA Kuu Jumatano ilitoa amri ya kuwazuia polisi kuweka vizuizi au kuzuia raia kufika katikati mwa jiji la Nairobi wakati wa maandamano.
Jaji Lawrence Mugambi alitoa amri hiyo ya muda kufuatia kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute baada ya jiji kufungwa wakati wa maandamano ya Saba Saba mnamo Jumatatu wiki hii.
Katiba Institute ilisema hatua ya polisi kufunga jiji kwa kutumia nyaya na kuwazuia raia kufika katikati mwa jiji ilikuwa kinyume cha sheria na ukiukaji wa haki na uhuru wao.
Shirika hilo lilisema kuwa bila amri ya korti, baadhi ya maafisa wa serikali ambao haikuwataja, wangebadilisha nchi kutoka uongozi wa kikatiba hadi ule wa unyanyasaji wa polisi wakati wa maandamano yajayo.
Shirika hilo lililalamika kuwa polisi walishiriki ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu na kuwanyanyasa raia Jumatatu.
“Inspekta Jenerali wa Polisi na Mwanasheria Mkuu wako kwenye hatari ya kufanya katiba isiwe na maana yoyote na kubadilisha demokrasia yetu kuwa iliyojaa udikteta,” ikasema Katiba Institute.
Jaji Mugambi alisema kuwa kesi hiyo ilifaa, akitambua kuwa kuzibwa kwa barabara bila notisi kulivuruga umma mnamo Jumatatu.
“Kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, natoa amri ya kuwazuia Inspekta Jenerali wa Polisi au afisa yeyote dhidi ya kuweka vizuizi na kuwazuia raia kuingia katikati mwa jiji la Nairobi,”
“Hawafai kuweka vizuizi au kuwazuia raia bila kutoa notisi ndipo raia nao wapange shughuli zao mapema,” akasema Jaji Mugambi.
Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, hawakuwa kortini wakati amri hiyo ilikuwa ikitolewa.
Hata hivyo, Jaji Mugambi alisema walikuwa wamewasilishiwa stakabadhi za kesi.
Kupitia wakili Malidzo Nyawa, Katiba Institute ilikuwa imesema kuwa kufungwa kwa barabara bila arifa wala taarifa kuliwavuruga Wakenya wakati wa maandamano.
Alimshutumu Inspekta Jenerali kwa kujitwalia mamlaka ya kuamua jinsi raia wanavyostahili kutekeleza haki zao za kikatiba.
Alisema shughuli za kikazi zilivurugwa baada ya barabara kufungwa, akitaja pia korti ambako kesi nyingi hazikuendelea baada ya wafanyakazi na mashahidi kushindwa kufika.
Wakili huyo alisema kuwa hatua hiyo inakiuka uamuzi wa Mahakama Kuu kuwa Inspekta Jenerali wa polisi hawawezi kupiga marufuku maandamano katikati mwa jiji.
“Hatua yao inaonyesha wanalenga kuhakikisha Wakenya wananyimwa nafasi ya kutumia barabara za umma bila ufafanuzi wowote,” akasema Bw Nyawa.
Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa Katiba Institute Nora Mbagathi, alisema uhuru wa kuandamana upo kwenye katiba ilhali serikali imekuwa ikiuzima kwa kutumia njia zisizo za kisheria.
“Umma hauwezi kuamka tu na kupata barabara zimefungwa na nyingine kuzingirwa kwa ua la nyaya.
Bila amri kutolewa na hii mahakama, uhuru wa raia utaendelea kuvurugwa,” akasema Bi Mbagathi.