Habari

Kaa na serikali yako lakini ujue wewe ni ‘One Term’, Gachagua aambia Ruto

Na KEVIN CHERUIYOT July 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumatano alipuuza madai kuwa upinzani unapanga njama ya kupindua serikali ya Rais William Ruto kupitia fujo na uharibifu wa mali.

Bw Gachagua alisema madai hayo yaliyotolewa na Rais Ruto hayana msingi na wao wanamakinika kuhakikisha anahudumu muhula moja pekee.

“Bw Rais hakuna mtu ambaye anataka kukuondoa mamlakani na hakuna yeyote anayetaka mamlaka kupitia njia zisizo za kikatiba. Bw Rais mimi na watu ninaoshirikiana nao watakuondoa Ikulu kupitia kura mnamo 2027,” akasema Bw Gachagua.

Kwa mujibu wa Bw Gachagua, madai ya Rais ni njama ya kuondoa umakinifu wa Wakenya kwenye dhuluma za polisi wakati wa maandamano.

“Tunataka uhudumu muhula wako mmoja wala hakuna kiongozi anayepanga kukutimua kupitia mapinduzi. Tunataka kupambana na wewe debeni mnamo 2027,” akaongeza.

Bw Gachagua alitetea tawala zilizopita akisema hazikuua au kuteka asasi za kikatiba jinsi Rais Ruto alivyofanya wakati huu.

“Serikali za Kibaki na Uhuru ziliongozwa na katiba na sheria. Hazikuteka asasi za kikatiba ili ziwafanyie kazi badala ya Wakenya wala utawala wao haukuwaua Wakenya au kuyajenga makanisa Ikulu,” akasema Bw Gachagua.

Hii ni baada ya Rais kuzua maswali kwa nini maasi kama haya sasa yanaendelezwa katika utawala wake ihali changamoto za nchi zilianza enzi za watangulizi wake.

“Moi alikuwa Rais wa Kenya kama tu Kenyatta, Kibaki na Uhuru. Mbona uadui huu? Mbona hawakufanya hivi kwa Kibaki au Uhuru? Wanalenga nini na ukosefu huu wa heshima? Sisi sote ni Wakenya,” akasema Rais Ruto.

Kiongozi huyo wa chama cha DCP alisema kuwa wimbi la maandamano nchini limekuwa likisababishwa na sera mbovu  na ushuru wa juu ulioanzishwa na serikali ya sasa.

Kuhusu uhuni ambao ulishuhudiwa hasa Ukanda wa Mlima Kenya,  aliyekuwa naibu rais alidai polisi walikuwa wakiwalinda wahuni waliojihami kuharibu biashara za watu ili alaumiwe.

Kiongozi huyo alitarajiwa kuondoka Jumatano jioni kuelekea Amerika ambako anatarajiwa kukutana na Wakenya na kuomba uungwaji mkono wao kuelekea siasa za 2027.

Upinzani umefichua kuwa unalenga kushirikiana na kikosi cha mawakili ili wawatetee vijana ambao walikamatwa wakati wa maandamano ya Saba Saba Jumatatu.