Habari

Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Abdul-halim Athman Hussein afariki

Na KALUME KAZUNGU July 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KADHI Mkuu wa Kenya Sheikh Abdul-halim Athman Hussein amefariki akiwa na miaka 55.

Familia, kupitia kakake mdogo, Sheikh Abubakar Athman Hussein ilithibitisha kifo chake kilichotokea majira ya alfajiri yapata saa saba kasorobo.

Alifariki akiwa nyumbani kwake mtaani Tudor, Kaunti ya Mombasa.

Kulingana na familia, Bw Abdul-halim, ambaye ni baba wa watoto watatu, alikuwa akiugua.

Mwaka 2024, Bw Abdul-halim alisafirishwa nchini India kwa matibabu, ambapo alipata nafuu hadi akarudi Kenya kuendelea na huduma yake.

Aidha, amekuwa akizuru hospitali ya Aga Khan mjini Mombasa mara kwa mara kufuatilizia hali yake ya afya.

Hata hivyo, kifo kilimpata akiwa nyumbani kwake Tudor Alhamisi.

“Ni huzuni kumpoteza kakangu, Kadhi Mkuu, Abdul-halim Athman Hussein leo alfajiri majira ya saa saba kasorobo. Amekuwa akiugua. Kama familia, jamii ya Kiislamu na Kenya kwa jumla, tumepoteza nguzo muhimu. Ndugu yangu ni mtu mpole, mwenye hekima,” akasema Bw Abubakar.

Aliongeza, “Yeye kila mara huendesha mambo yake kwa kuzingatia haki. Ninamfahamu kuwa kiongozi mtaratibu wa mambo. Ni mwenye tabia nzuri na mtu wa watu. Tulitarajia afanye mengi makuu zaidi ila kifo kikakatiza ndoto yake.”

Binamuye, Bwanaobo Mohamed, alimtaja Bw Abdul-halim kuwa msomi mwenye tajiriba hasa katika masuala ya dini ya Kiislamu, mpole na karimu.

Familia ya Kadhi Mkuu Sheikh Abdul-halim Athman Hussein ikimuomboleza nyumbani kwake Tudor, Mombasa, Alhamisi. Picha|Kevin Odit

“Binamu yangu namfahamu kuwa mpole kama babake, Sheikh Hussein Athman almaarufu Ustadh Bahuseni wa Malindi. Licha ya mara nyingi kuwepo kwa tofauti za kimadhehebu katika dini, yeye alihakikisha anafanya kazi na kupatanisha kila mtu,” akasema Bw Mohamed.

Aliongeza kuwa Bw Abdul-halim katu hakujali tofauti za kidini, kidhehebu na kikabila.

“Yaani alileta umoja, amani na uwiano kwa wote. Ameacha pengo ambalo ni vigumu kulijaza. Mola amlaze pema peponi,” akasema Bw Mohamed.

Akituma risala zake za rambirambi kufuatia kifo cha Kadhi Mkuu, Abdul-halim Athman Hussein, Jaji Mkuu Martha Koome alisema kifo kimeipokonya Kenya mtu muhimu

“Sheikh Abdul-halim Hussein Athman alitumikia mahakama na Wakenya kwa bidii, uwajibikaji, unyenyekevu na uadilifu,” akasema Bi Koome katika ujumbe wake.

Mwili wa mwendazake uko nyumbani kwake, Tudor huku mipango ya mazishi ikiendelea.

Familia imesema maombi yatafanyika baadaye alasiri katika Msikiti Nuru eneo la Bondeni kabla ya mazishi kufanyika kwenye makaburi ya Waislamu ya Kikowani, eneobunge la Mvita, kaunti ya Mombasa.

Miongoni mwa waliotuma rambirambi ni pamoja na Mwenyekiti wa Muungano wa Wanahabari Waislamu nchini Kenya (Muslim Media Practitioners of Kenya (MMPK) Juma Namlola aliyeitakia familia, jamaa, marafiki na Waislamu wote faraja wakati huu wa maombolezo.

Waombolezaji wafika nyumbani kwa Kadhi Mkuu Sheikh Abdul-halim Athman Hussein. Kadhi huyo ameaga dunia baada ya kuugua kwa muda. Picha|Jurgen Nambeka

“Sheikh Abdulhalim Athman Hussein alikuwa kiongozi mashuhuri wa Kiislamu, mcha Mungu, mwenye hekima na mwenye kujitolea kwa hali na mali katika kuongoza Mahakama za Kadhi na kuimarisha uelewa wa sheria za Kiislamu nchini Kenya. Kupitia maisha yake ya ibada, elimu na uadilifu, aligusa nyoyo za wengi na kuwahudumia Waislamu kwa moyo wa unyenyekevu na huruma. Taifa limepoteza nguzo muhimu ya uadilifu na mshikamano wa kidini,” akasema Bw Namlola.

Katibu Mshirikishi wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu Nchini (CIPK) tawi la Lamu, Bw Mohamed Abdulkadir alimtaja Bw Abdul-halim kuwa mtu mwema aliyeleta amani, umoja, uwiano na utangamano katika Usislamu, dini na makabila yote bila ubaguzi.

Bw Abdul-halim aliteuliwa na Tume ya Mahakama nchini Kenya (JSC) mnamo Julai 2023 kuhudumia wadhfa wa Kadhi Mkuu wa Jamhuri ya Kenya, hivyo kujaza pengo la Sheikh Ahmed Muhdhar aliyekuwa amestaafu 2022 baada ya kuhudumu kwa miaka 12.