Tahariri

TAHARIRI: Malumbano kati ya Rais, Rigathi hatari kwa nchi

Na MHARIRI MKUU July 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wanastahili kufahamu Wakenya hawataki kuzamishwa kwenye tofauti zao za kisiasa bali wanataka huduma bora.

Jana, kulikuwa na majibizano makali kati ya Rais Ruto na Bw Gachagua kutokana na wimbi la maandamano ambalo limegubika nchi katika siku za hivi majuzi.

Rais Ruto alisema maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini yana ajenda kuu ya kumngóa mamlakani kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Gachagua naye alidai maafa, uporaji na uharibifu wa mali ambao umekuwa ukishuhudiwa Ukanda wa Mlima Kenya, unafadhiliwa na serikali.

Aliyekuwa naibu rais hata hivyo, alijitetea kuwa hakuna mwenye nia ya kutumia njia za mkato kumbandua Rais Ruto mamlakani.

Malumbano kati ya wanasiasa haya yamefaulu tu kupalilia ukabila badala ya kujenga umoja wa nchi.

Cheche za kikabila kati ya mirengo inayounga mkono serikali na ile inayounga upinzani mitandaoni zinaonyesha tu jinsi taifa linaelekea kusambaratishwa na tofauti kali kati ya wanasiasa hawa wakuu.

Rais Ruto na Bw Gachagua ni wanasiasa tajiri ambao hawawezi kukosa mlo au kukosa wanachotaka maishani kwa sababu pesa wanazo.

Kwa upande mwingine, wanawagonganisha Wakenya ambao hawana mbele wala nyuma na hutegemea wema na kudura za mwenyezi Mungu kuishi.

Kwa sasa, wanaogua makovu ya maandamano ni Wakenya ambao mali yao iliporwa na familia 31 zilizopoteza wapendwa wao kutokana na ukatili wa polisi.

Hata maandamano yenyewe yasingekwepo serikali ingetimiza ahadi tele ilizotoa na kuwaondoa Wakenya kwenye lindi la umaskini?

Walipotwaa uongozi wa nchi 2022, Rais na Bw Gachagua walitoa ahadi nyingi na hakuna mmoja wao ataepuka lawama kutokana na ugumu wa maisha kwa sasa nchini.

Hata wakati Bw Gachagua alikuwa serikalini kabla ya kungátuliwa Oktoba mwaka jana, changamoto hizi zilikwepo lakini hakufungua kinywa chake.

Sasa ndiyo huyo kwenye vyombo vya habari akiwachochea Wakenya dhidi ya serikali ilhali alikwepo wakati makato ya Bima Mpya ya Kijamii (SHA) yalipoanzishwa, mradi wa nyumba za gharama nafuu pamoja na miradi mingine iliyopandisha ushuru.

Itawanufaisha nini Rais na Bw Gachagua iwapo nchi hii itachukua mwelekeo wa siasa za kikabila na kusambaratika raia wakiendelea kuumia?