Makala

Utafiti: Wanaume wengi wanaumia kimya kimya na tatizo la mkojo kuvuja

Na CECIL ODONGO July 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

IMEBAINIKA kuwa zaidi ya nusu ya wanaume ambao wamefikisha umri wa miaka 60, hawamakinikii tatizo la kibofu cha mkojo kuvuja na kushindwa kudhibiti haja ndogo.

Utafiti ambao uliendeshwa na Kituo cha Sayansi cha Boston na Kampuni ya utafiti ya Talker, ulifichua kuwa asilimia 60 ya wanaume huchukua tatizo la kushindwa kuhimili mkojo uzeeni kama jambo la kawaida badala ya kuenda kusaka matibabu.

Ni asilimia 46 pekee ambayo huendea matibabu nayo asilimia 43 huamua kuvaa nepi wakichukulia tatizo hilo kama mabadiliko ya maisha yanayotokana na uzee.

Hii ni licha ya kuwa si hakikisho kuwa ukiingia uzeeni utaandamwa na mkojo kuvuja, mara nyingi waliokonga sana wakiathirika.

Wengi wa wanaume walioulizwa pia walisema hawamakinikii matibabu wakihofia aibu inayotokana na kutafuta matibabu na jinsi watakavyochukuliwa.

Isitoshe wengi walisema hawafahamu iwapo kuna matibabu ya tatizo hilo na huamua kujinyamazia.

Ingawa hivyo, watafiti wanaamini kuwa iwapo kutakuwa na mahamasisho kuhusu njia ya matibabu ya mwanaume kushindwa kudhibiti mkojo, wengi watajiepusha na tatizo hili.

Hii ni kwa sababu uzee pekee si hakikisho kuwa ugonjwa huu huwaandama wanaume wazee na haufai matibabu hata katika kiwango hicho.

“Tatizo la kushindwa kudhibiti mkojo halifai kuvumiliwa na wanaume au wao kujificha kwa kuhofia aibu. Kuna aina mbalimbali za matibabu ikiwemo kufanyiwa upasuaji kupata suluhu ya muda mrefu ndiyo maana wengi ambao wanakabiliana na tatizo hili wanastahili kuzungumza na daktari au mhudumu wa afya,” akasema mtaalamu wa masuala ya kimatibabu Boston, Dkt Ron Morton.

Kando na hili la mkojo kuvuja, wanaume wengi imebainika kwenye tafiti za awali kuwa hawaendei vipimo na huja kugundua baadaye kuwa wana maradhi mbalimbali sugu.

“Wanaume wachukue suala la afya yao kwa uzito jinsi umri unavyosonga. Hii itawasaidia kufahamu mbinu za matibabu wanazohitaji pamoja na kuzoa kuzungumza na madaktari kuhusu changamoto zao,” akaongeza Dkt Morton.