Makala

Kaunti yashtaki mkazi kwa kudai umiliki ardhi iliyojengwa mji

Na  PIUS MAUNDU July 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Wasiwasi umekumba wafanyabiashara katika Mji wa Kaumoni, Kaunti ya Makueni, kufuatia mzozo wa muda mrefu kuhusu umiliki wa kipande cha ardhi cha ekari tatu ambapo mji huo unapatikana, ambao sasa umefika mahakamani.

Serikali ya Gavana wa Makueni, Mutula Kilonzo Junior, imemshtaki Henry Mwongela, jirani wa mji wa Kaumoni, kuhusu umiliki wa ardhi hiyo anayodai kuwa ni yake.

Ardhi inayozungumziwa imesajiliwa kama Ukia/Kaumoni/75.

Jaji Elijah Obaga wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Kaunti ya Makueni ameweka Julai 29 kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Bw Mwongela. Mbali na kumiliki hati miliki ya ardhi hiyo inayozozaniwa, Bw Mwongela pia ni msimamizi wa mali ya baba yake marehemu, Samuel Kinyili Nzou.

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani, Ukia/Kaumoni/75 ina ukubwa wa ekari 1.7. Hata hivyo, kesi hiyo inadai kuwa Mji wa Kaumoni umekua kwa miaka mingi na kuchukua ekari 1.4 kutoka kwa ardhi jirani iliyosajiliwa kama Ukia/Kaumoni/76. Thamani ya ardhi inayozozaniwa, kulingana na tathmini ya mwaka 2023, iliyowasilishwa mahakamani na Bw Mwongela, ni Sh11.5 milioni.

Wakili wa Kaunti ya Makueni, Stanley Nthiwa, amemshtaki Bw Mwongela pamoja na Priscilla Mueni, mjane wa kaka yake marehemu Bw Mwongela; Msajili wa Ardhi Kaunti ya Makueni, Roselyn Soo; na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor. Wametajwa kama washtakiwa wa pili, wa tatu, na wa nne mtawalia.

Bw Nthiwa anamlaumu Bw Mwongela kwa kupata hati miliki ya Ukia/Kaumoni/75 kwa njia ya udanganyifu. Katika stakabadhi za mahakama zilizoonekana na Taifa Leo, anataka mahakama iamuru Bw Mwongela aikabidhi serikali ya kaunti kipande kizima cha ardhi ambapo Mji wa Kaumoni umesimama bila masharti yoyote.

La kushangaza ni kuwa Bi Soo ambaye ofisi yake ilihusika moja kwa moja kutoa hati hiyo amekana madai ya Bw Mwongela.

‘Washtakiwa wa tatu na wa nne wanathibitisha kuwa ardhi inayozozaniwa ilitengwa kwa ajili ya Soko la Kaumoni chini ya Baraza la Makueni wakati wa mpango wa upimaji ardhi mwaka 1975. Haijulikani ni kwa namna gani ardhi hiyo ilisajiliwa kwa jina la Samuel Kinyili Nzou. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa inamilikiwa na serikali ya Kaunti ya Makueni na si mshtakiwa wa kwanza au wa pili. Washtakiwa wa tatu na wa nne wanapenda kusema kuwa huenda kulikuwa na makosa wakati wa maandalizi ya hati miliki, jambo ambalo linajutiwa sana na halikukusudiwa,’ alisema Msajili wa Ardhi kupitia kwa Wakili wa Serikali Lydia Lung’u.

Hata hivyo, Bw Mwongela amekanusha madai ya udanganyifu katika upatikanaji wa ardhi hiyo. Anasema katika hati za mahakama kuwa ardhi hiyo ilikuwa ya baba yake marehemu, Mzee Kinyili.

Anadai kuwa wakati wa upimaji wa ardhi mwaka 1975, iliyokuwa Baraza la Kaunti ya Makueni wakati huo ilitoa ardhi kwa wawekezaji waliovutiwa na ardhi ya Ukia/Kaumoni/75, kutokana na ukaribu wake na Kanisa Katoliki Kaumoni na Shule ya Sekondari ya Kaumoni. Kwa miaka mingi, eneo hilo liligeuka kuwa soko lenye shughuli nyingi likiwa na maduka, mikahawa, na mashine za kusaga mahindi.

Ili kuimarisha kesi yake dhidi ya serikali ya Gavana Kilonzo Jnr, Bw Mwongela amejumuisha ushahidi kutoka kwa mzee mmoja wa miaka zaidi ya 80, anayesema kuwa alikuwa miongoni mwa wazee waliowaongoza maafisa wa serikali wakati wa upimaji ardhi wa mwaka 1975.

‘Ardhi inayozozaniwa ni mali ya Mzee Kinyili. Alitarajia Baraza la Kaunti ya Makueni kununua ardhi hiyo kutoka kwake ili kujenga soko. Hata hivyo, baraza ilisema haingeweza kutumia pesa kununua ardhi isiyo na hati miliki,’ alisema Mzee John Luvai Kisilu katika hati yake ya kiapo.

Miaka kadhaa baada ya Mzee Kinyili kufariki, Bw Mwongela alipata hati miliki ya ardhi hiyo mwaka 2019 kwa jina la baba yake, na baadaye akaihamishia kwake kupitia urithi.

Bw Mwongela anasisitiza kuwa upatikanaji wa hati hiyo ulikuwa halali.

‘Mchakato wa kupewa hati na usajili wa ardhi hiyo kwa jina la Samuel Kinyili Nzou ulikuwa wa kisheria na ulizingatia kumbukumbu sahihi zilizokuwepo katika ofisi ya mshtakiwa wa tatu. Mshtakiwa wa tatu asingeweza kutoa na kusajili hati hiyo bila kumbukumbu zinazoonyesha kuwa ni mali ya marehemu Samuel Kinyili Nzou,’ alisema Bw Mwongela kupitia wakili wake Sichangi Nyongesa.

Mzozo huu wa umiliki wa Mji wa Kaumoni sasa unatarajiwa kuchelewesha inayoendelea ya kuweka lami Barabara ya Tawa–Itangini, inayopita katikati ya eneo hilo.