Mwongozo wa urithi wa mali ya marehemu asipoacha wosia
Mtu akifariki dunia, mali yake hugawanywa kwa warithi wake kupitia mchakato wa urithi. Hii inaweza kufanyika kupitia wosia au bila wosia. Kuna mambo mengi na sheria mbalimbali ambazo mahakama huzingatia katika urithi bila wosia ili kuhakikisha mali inagawa kwa haki kwa warithi.
Sheria hizi zimetolewa chini ya Sheria ya Urithi, Sura ya 160 ya Sheria za Kenya.
Sheria za urithi bila wosia nchini Kenya huzingatia tu mke/mume na jamaa wa damu wa marehemu, ambapo watoto wa marehemu hupatiwa kipaumbele kuliko jamaa wengine wa damu.
Ni muhimu kueleza kuwa watoto wote wa marehemu, bila kujali jinsia au umri, wanachukuliwa kuwa sawa mbele ya sheria. Watoto wa kuasili na waliozaliwa nje ya ndoa pia wanalindwa kikamilifu chini ya Sheria ya Urithi.
Kenya inatambua ndoa za mke mmoja na ndoa za wake wengi, hivyo basi sheria za urithi wa bila wosia nchini Kenya zinatoa mwongozo kwa familia zilizoanzishwa chini ya mifumo yote miwili ya ndoa.
Endapo marehemu ameacha mke au mume na mtoto au watoto, mke/mume aliyebaki hai atapata mali ya matumizi binafsi na ya nyumbani ya marehemu. Ni haki yake kutumia mali ya urithi kwa maisha yake yote, lakini si umiliki wake.
Hii inamaanisha kuwa mke/mume aliyebaki hai anaweza kutumia na kufaidika na mali hiyo hadi atakapofariki, ambapo mali hiyo itapatiwa watoto kama warithi.
Hata hivyo, haki hii ya maisha inakatika mara moja iwapo mke/mume huyo atafunga ndoa tena.
Wakati wa maisha yake, mke/mume aliyebaki hai ana uwezo wa kugawa sehemu au mali yote kama zawadi kwa watoto wa marehemu. Iwapo mtoto ataona kuwa mke/mume aliyebaki hai ametumia vibaya au amekataa kutumia mamlaka hiyo kwa haki, anaweza kuomba mahakama apatiwe sehemu yake.
Mahakama huzingatia mambo kadhaa kabla ya kutoa uamuzi, yakiwemo: Aina na thamani ya mali ya marehemu, hali ya kifedha na mahitaji ya mwombaji na ya mke/mume aliyebaki hai, zawadi zozote zilizotolewa awali na marehemu kwa mwombaji,
Tabia ya mwombaji kwa marehemu na mke/mume aliyebaki hai, na hali ya warithi wengine wote.
Ikiwa mke/mume wa marehemu amefariki au kuolewa/ kuoa tena mali iliyosalia hugawiwa mtoto au watoto waliobaki, kulingana na maagizo yaliyotolewa au uamuzi wa mahakama.
Ikiwa marehemu hakuacha mume/mke bali mtoto au watoto kadhaa mali yote ya marehemu huwa ya mtoto mmoja aliye hai au kugawanywa kwa usawa kati ya watoto waliobaki hai.
Kifungu cha 40 cha Sheria ya Urithi kinashughulikia urithi katika ndoa za wake wengi. Kifungu hiki kinasema kuwa, mtu mwenye wake wengi akifariki, mali ya matumizi binafsi na ya nyumbani pamoja na mali iliyobaki itagawanywa kwa kila mke.
Hii ufanyika kulingana na idadi ya watoto katika kila familia ambapo kila mtoto na kila mke aliyebaki hai huhesabiwa kama kitengo kimoja ndani ya familia hiyo.
Kama ilivyo katika ndoa ya mke mmoja, wake waliobaki hai katika ndoa ya wake wengi wanapewa mali ya matumizi binafsi na ya nyumbani ya marehemu ya famili yao, na haki ya kutumia mali iliyosalia kwa maisha yao yote, haki ambayo huisha iwapo wataolewa tena.