Habari za Kitaifa

Hofu SHA ikifuta leseni za hospitali za Level 3, 4 kulaza wagonjwa

Na  ANGELA OKETCH July 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HOSPITALI kadhaa kote nchini zimeshindwa kulaza wagonjwa baada ya data kuhusu idadi ya vitanda iliyojazwa kwenye tovuti ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kubadilishwa kuwa sufuri kuashiria haziwezi kuwa na wagonjwa wa kulazwa.

Hatua hiyo ya hivi majuzi imeathiri vituo vya afya vya Level 3 na 4 vinavyohudumu ngazi ya chini ya huduma ya afya ya msingi kwa idadi kubwa ya Wakenya wanaohitaji matibabu.

Wamiliki na maafisa wa hospitali waliozungumza na Taifa Leo walielezea sintofahamu na kunganyikiwa huku wakilazimika kuwarudisha wagonjwa licha ya kuwa na vitanda na wafanyakazi waliofuzu tayari kuhudumu.

Mmiliki wa hospitali iliyopo barabara ya Lang’ata, Nairobi, aliyelipia leseni yake Sh30,000, aligundua licha ya kujaza nafasi ya vitanda 45 jinsi leseni yake ilivyoashiria, mfumo wa SHA unaonyesha hakuna nafasi ya kuwalaza wagonjwa.

“Sielewi. Nilienda kwa Baraza la Madaktari Nchini (KMPDC) kuhusiana na suala hilo maadamu kwa wiki moja na nusu zilizopita, sijaweza kuwalaza wagonjwa, hususan wanawake wanaohitaji huduma za kuzaa, lakini nikaelezwa afisa aliyepaswa kunihudumia yupo likizo,” alisema akichelea kutajwa.

Mmiliki wa hospitali nyingine alisema tovuti ya SHA inaashiria kituo chake hakina nafasi ya vitanda vya kuwalaza wagonjwa na baada ya kufuatilia kwa Baraza, waliambiwa leseni yake ya 2025 haipatikani kwenye sajili.

“Mbona tovuti isome sufuri ilhali leseni yangu inasema nafasi ya vitanda 47. Baraza halijawasiliana licha ya kulipia leseni ya Kituo cha Level 4. Kuwa na vitanda sufuri kunamaanisha hospitali haina uwezo. Nani anaamua haya? Mawasiliano haya yalitumwa wapi?” alisema akichelea kutajwa.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Muungano wa Hospitali za Kibinafsi Mashinani na Mijini, Dkt Brian Lishenga, alisema vituo hivyo vilipatiwa leseni na (KMPDC) hususan kutoa huduma za wagonjwa wa kulazwa.

“Kutokana na rekodi za baraza, mwanzoni hospitali zilipatiwa leseni za kuwalaza wagonjwa, idadi mahsusi ya vitanda ikionyeshwa kwenye leseni zao. Hata hivyo, sasa, kuna madai kuwa hospitali za Level 3 na 4 hazifai kuwa na vitanda. Vipi kuhusu wagonjwa wanaokwenda hospitali hizi?”alihoji.