Polisi waandama mhalifu anayebaka wanawake kisha kuwaua
MHALIFU sugu sasa anaandamwa na polisi katika Kaunti ndogo ya Gem-Yala, Kaunti ya Siaya, kutokana na misururu ya mauaji ambayo yamekuwa yakishuhudiwa kwa miezi katika eneo hilo.
Mauaji hayo yamezua hofu mno katika eneo hilo, wengi sasa wakilaani ukatili huo na kuhofia maisha yao na ya watoto wao.
Kamanda wa Polisi wa Gem Charles Wafula, alisema kuwa mshukiwa wa mauaji hayo ni Charles Onyango maarufu kama ‘Kwa’ ambaye anaandamwa na maafisa wa usalama.
Mkuu huyo wa polisi aliambia Taifa Leo kuwa operesheni kali inaendelea ya kumkamata Onyango ambaye ameingia mafichoni.
“Tunafuata njia zote ambazo zitatuwezesha kumfikia kutoka kwenye maficho yake. Tunaomba raia yeyote ambaye ana habari kumhusu, apige ripoti kwenye kituo cha polisi ili kusaidia katika uchunguzi,” akasema Bw Wafula.
Alisema kuwa mshukiwa huyo amekuwa akiwalenga sana wanawake na wasichana wadogo na huwadhulumu kingono kabla ya kuwaua.
Hofu zaidi ilizuka kuhusiana na misururu ya mauaji hayo baada ya mwili wa mwanamke na viganja vya mikono, vilivyokuwa vimeanza kuoza kupatikana ndani ya choo.
Miili hiyo ilipatikana kwenye kijiji cha Kachola mnamo Julai 1 na kuzua hofu na taharuki zaidi miongoni mwa wenyeji.
Inakisiwa mwili huo ni wa Elizabeth Atieno Ochieng’, 15, mwanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Uranga, Gem Mashariki.
Aliuawa mnamo Julai 3 kisha mwili wake ukakatwa vipande vipande. Bw Wafula alisema kuwa ushahidi wote unaonyesha kuwa Bw Onyango ndiye alihusika na mauaji hayo.
“Kanda ya CCTV zinaonyesha mshukiwa akiwa na wasichana hao wawili mjini Yala mnamo Julai 3. Wasichana hao wametambuliwa kama Elizabeth Atieno na dadake mdogo ambao walikuwa wameenda kuchukua sare zao kwenye mojawapo ya maduka mjini Yala,” akasema Bw Wafula.
Baada ya kuondoka mjini Yala, dadake Elizabeth alienda kuteka maji kutoka kwa boma moja jirani lakini aliporudi hakumpata dadake na Bw Onyango alikowaacha.
Tangu siku hiyo familia yao ilikesha ikimtafuta Elizabeth bila ufanisi wowote.
Mzee wa Kijiji, Peris Ngesa, baadaye alihisi uvundo kutoka choo kimoja karibu na nyumba yake ndipo akapata mwili wa Bi Achieng’ ukiwa ndani.
Aliwaita maafisa wa polisi ambao waliuondoa mwili huo huku wengi wakizua maswali kuhusu kiini cha unyama huo.
Mshukiwa huyo pia anahusishwa na mauaji ya Veronica Odongo, 46, ambaye aliuawa mnamo Julai 5 na mwili wake kutupwa Mto Yala.
Pia anahusishwa na kuwaua Ema Akinya, 17, mwanafunzi wa Yala Township mnamo Mei 26 na Angel Mitchel, mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Kasagam.