Habari

Washukiwa wakuu wa uvamizi wa Hospitali Kitengela wanaswa

Na STANLEY NGOTHO July 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIKU sita baada ya wahuni kuvamia Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela, Kaunti ya Kajiado, wakati wa maandamano ya ukumbusho wa Siku ya Saba Saba, wapelelezi wa idara ya kuchunguza jinai (DCI) wamewakamatwa washukiwa wawili wakuu.

Siku hiyo, Julai 7, waandamanaji waliteka hospitali hiyo kwa zaidi ya saa sita baada ya mwenzao Brian Kimutai, 21, kufariki baada ya kufikishwa hapo kwa matibabu.

Walizua vurugu na hofu hospitalini humo, hali iliyowalazimisha wahudumu wa afya na wagonjwa kukimbia ili kujiokoa. Mali ya thamani kubwa iliharibiwa katika Hospitali hiyo ya Kaunti Ndogo ya Kitengela, katika rabsha hizo.

Mnamo Jumamosi, maafisa wa DCI kutoka Nairobi wakisaidia na wenzao wa Kitengela waliwakamatwa washukiwa wawili; mmoja mwenye umri wa miaka 28 na mwingine mwenye umri wa miaka 21.

Inasemekana kuwa mshukiwa mwenye umri wa miaka 21 alikuwa rafiki wa karibu wa mwendazake Kimutai.

Kulingana na picha za kamera za usalama (CCTV), zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii, wawili hao walionekana wakivamia na kuharibu mali katika hospitali hiyo.

Mshukiwa mwenye umri wa miaka 21 ndiye alikuwa wa kwanza kukamatwa Ijumaa jioni dakika chache baada ya kuondoka hospital moja ya kibinafsi alikolazwa tangu Jumatatu usiku.

Wahudumu wa boda boda walioongea na Taifa Leo walisema maafisa waliokuwa wakisafiri kwa gari aina ya Subaru Forester walimchukua mshukiwa huyo akiwa kwenye lango la hospitali hiyo.

“Tulikuwa tukimfuatilia mshukiwa kwa muda wa saa 24,” akasema afisa mmoja wa upelelezi ambaye aliomba tulibane jina lake, kwani haruhusiwi kuzungumza na wanahabari.

Kulingana na wapelelezi wa DCI, mshukiwa mkuu wa uhalifu huo alikamatwa katika maficho yake mjini Kitengela Jumamosi jioni.

Baada ya kukamatwa kwake, aliwaelekeza wapelelezi katika makazi yake katika kitongoji cha Noonkopir ambako kofia na jaketi aliyovaa siku ya uvamizi wa hospitali zilipatikana.

Mkuu wa DCI Kitengela Joseph Indeke aliambia Taifa Leo kwamba wanaendelea kupiga hatua katika jitahada zao za kuwakamata washukiwa.

“Tunawasaka washukiwa wengine. Tutanasa hivi karibuni. Wajue kwamba wanaweza kutorokana lakini hawawezi kujificha,” akasema Indeke.