Habari za Kitaifa

Wandani wa Ruto Rift Valley waunga amri ya waandamanaji kupigwa risasi mguuni

Na OSCAR KAKAI July 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANDANI wa Rais William Ruto Ukanda wa Bonde la Ufa wamemtetea kuhusu kauli yake kuwa waandamanaji walengwe na wapigwe risasi mguuni iwapo watakuwa wakishiriki uporaji na uharibifu wa mali.

Mnamo Jumatano wiki jana, Rais aliamrisha kuwa polisi wawapige waandamanaji risasi miguuni, hasa wale ambao wanashiriki uporaji na uharibifu wa mali.

Kupigwa risasi kutalenga kuwalemaza kisha washtakiwe mahakamani wakiwajibikia vitendo vyao.

Alisema hayo baada ya watu 38 kuuawa kwenye maandamano siku ya Saba Saba, mauaji yaliyolaaniwa ndani na nje ya nchi.

Kauli ya rais imezua maoni kinzani huku mashirika ya kijamii yakimkashifu nao baadhi ya viongozi wa kisiasa wakimuunga mkono.

Wabunge Dkt Samuel Moroto (Kapenguria), Peter Lochakapong (Sigor), Seneta wa Pokot Magharibi Julius Murgor na Mbunge Mwakilishi wa Pokot Magharibi Rael Kasiwai, wote walisema rais lazima aheshimiwe na apewe muda wa kutimiza ajenda zake kwa Wakenya.

“Huenda rais alijikwaa ulimi na hakumaanisha polisi waue raia. Kama kiongozi ambaye amechaguliwa, lazima aheshimiwe,” akasema Dkt Moroto.

Mbunge huyo alishangaza zaidi kwa kudai kuwa kila rais lazima ahudumu mihula miwili akisisitiza Rais Ruto naye lazima akamilishe muhula wake.

“Kama marais wengine walimaliza mihula yao, mbona Rais Ruto asimalize? Kama amekosea tunastahili kumwaambia ukweli badala ya kumkashifu na kumfanyia maandamano,” akaongeza.

Bw Lochakapong alisisitiza kuwa amri ya kuwapiga risasi waandamanaji waporaji miguuni haimanishi kuwa polisi sasa wawapige risasi kiholela.

“Kile ambacho rais alisema kipo kwenye sheria na hakifai kufasiriwa vibaya. Rais hawezi kusema kitu bila kutathmini athari yake navyo vyombo vya usalama vinastahili kuachwa vitekeleze wajibu wao,” akasema mbunge huyo.

Bw Murgor aliunga mkono matamshi ya Rais akisema lazima polisi wapambane na wahalifu.

“Wanahitajika kupelekwa kortini ili kujibu mashtaka kwa sababu wengi wao huiba wakiwa wamejihami kwa mawe na marungu. Japo kuna haki ya kuandamana, hawa wamevuka mipaka,” akasema huku akitoa Wakenya waache maandamano kwa sababu yalikuwa yakisababisha taharuki ya kisiasa nchini.

“Kuna haki ya kuandamana lakini uhuru huo umetumika vibaya kwa sababu hata haki za watu wengine sasa zinavurugwa. Kuna haja gani ya maandamano ilhali watu wanapoteza mali na maisha yao?”

“Nafasi nyingi za kazi zimepotea na sasa ni hasara huku wanaodhamini ghasia hizo na waporaji wakinufaika,” akaongeza Bw Murgor.

Wanasiasa hao walikuwa wakizungumza baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo eneo la Kambi Karaya katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Kauli ya Rais Ruto kuhusu kupigwa risasi kwa waandamanaji aliyoitoa Julai 9, ilikuja huku Shirika la Kitaifa la Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR) likisema watu 38 wameaga dunia na wengine 107 kujeruhiwa wakati wa maandamano hayo.