Habari

IEBC mpya yaingia darubini ya Gen Z waliofanya mitandao kuwa na nguvu kuliko vyama

Na NICHOLAS NJOROGE July 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MWAKA mmoja uliopita, Gen Z nchini Kenya walimshinikiza Rais kulegeza msimamo kuhusu mswada wa fedha.

Sasa, wanawalenga makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Makamishna saba wa IEBC walioteuliwa wiki iliyopita hawakurithi shughuli za uchaguzi wa Kenya pekee bali wameingia moja kwa moja kwenye darubini ya kizazi kilichovamia Bunge, kikaangusha waziri wa fedha, na kugeuza mitandao ya kijamii kuwa na nguvu kuliko vyama vya kisiasa.

“Tulivunja serikali nzima kwa kutumia simu zetu,” anasema Cynthia Achieng, 22, mwanafunzi wa sheria, huku akitazama video alizohifadhi kwenye TikTok kutoka maandamano ya Juni 2024 yaliyobadilisha Kenya milele. “Sasa tunawaangalia hawa makamishna hatua kwa hatua.”

Timu hiyo mpya inayoongozwa na mwenyekiti Erastus Edung Ethekon, pamoja na makamishna Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol na Fahima Araphat Abdallah, iliingia ofisini baada ya siku 906 tangu kuondoka ofisini kwa watangulizi wao.

Lakini hii si Kenya ile ile iliyowapokea watangulizi wao.

Kati ya Juni na Julai 2024, vijana wa Kenya waliandika upya mbinu za ushiriki wa kisiasa kwa wakati halisi.

Wakiwa na simu za kisasa na intaneti pekee, walitafsiri Mswada tata wa Fedha wa 2024 kwa lugha za wenyeji, wakatumia ChatGPT kufafanua sera tata za ushuru, na hata kuanika nambari za simu za wanasiasa katika kampeni yao.

Serikali ya Rais William Ruto ilipojaribu kusukuma mbele ongezeko la ushuru, Gen Z hawakulalamika tu bali waliandamana.

Waandamanaji walirusha mubashara makabiliano na polisi.

Tofauti na maandamano ya zamani yaliyoongozwa na wanasiasa, haya hayakuwa na viongozi wa kawaida, hayakuwa na miungano ya vyama, na hayakuwa na uvumilivu kwa “miungu wa siasa”.

“Raia wanataka mchakato wa usajili wa wapigakura ambao ni rafiki kwao,” alisema Dkt Ekuru Aukot aliyeshuhudia maandamano haya yakibadilisha taswira ya siasa nchini.

“Lakini hawa vijana wanataka kitu ambacho vizazi vya zamani havikuwahi kudai, uwazi wa mara moja.”

Wakati makamishna wa IEBC walipoteuliwa mwaka 2021, waandamanaji wa sasa walikuwa wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakitafuta ajira.

Wengi wao walinufaika na sera za elimu bila malipo, wakiwa na matumaini ya maisha bora.

Badala yake, walikumbana na ukosefu wa ajira wakiwa asilimia 67 ya raia, huku wakitazama wanasiasa wakiishi maisha ya kifahari wakati raia wa kawaida walikabwa na mfumuko wa bei.

“Sisi kama vijana wa Kenya, tunachotaka ni mfumo wa uwazi, unaosikiliza matatizo yetu na usiodhibitiwa na wanaotetea serikali. IEBC mpya lazima ifanye kazi kwa uhuru,” alisema Sammy Oluoch, 24, mmoja wa wanaharakati waliochangia kuangushwa kwa Mswada wa Fedha 2024.

IEBC ya awali ilifanya kazi kimyakimya, ikitoa maamuzi nyuma ya pazia bila ukaguzi wa umma lakini sasa Gen Z wameonekana kuifuatilia kwa karibu.

Wakati huu, makamishna wanakutana na kizazi kilichounganishwa kidijitali, ambacho tayari kimegeuza majengo ya serikali kuwa matangazo ya moja kwa moja duniani kote, na kuwafanya mawaziri kuwa majina ya kawaida mitandaoni na kwa sababu mbaya.
Wakati huu wa uteuzi wa IEBC si rahisi.

Kwa zaidi ya miaka miwili, IEBC haikuwa na makamishna, hali ambayo mahakama ilisema inafanya maamuzi ya tume hiyo kuwa batili.

Athari zimeanza kuonekana: wakazi wa Banisa hawajapata mwakilishi tangu Mbunge Kulow Maalim alipofariki Machi 2023, kwa kuwa uchaguzi mdogo haukuweza kufanyika.

Zaidi ya hayo, Kenya imechelewa kuchunguza upya mipaka ya maeneo bunge tangu Machi 2012. Katiba inataka ukaguzi wa kila baada ya miaka 8-12, na muda huo uliisha Machi 2024.

Bila makamishna, zoezi hilo muhimu haliwezi kufanyika.

Lakini mageuzi ya taasisi hayawezi kuwatosheleza vijana ambao tayari wameonyesha uwezo wa kubadilisha uhalisia wa kisiasa kwa kutumia harakati za kidijitali.

Katika maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha, vijana hawakupinga tu sera waliunda mifumo mbadala ya taarifa, mitandao ya uhakiki wa ukweli kwa wakati halisi, na mbinu za uratibu zilizoepuka vyombo vya habari vya kawaida.

“Kizazi hiki hakivumilii kabisa uzembe,” Achieng anasisitiza.

“Tumekulia kwenye taarifa za papo kwa hapo, tunataka uwajibikaji papo kwa papo. Makosa yoyote ya IEBC tutayaibua—mubashara, kwa wakati huo huo, na ushahidi kamili.”

Maandamano yalionyesha kuwa takriban asilimia 60 ya vijana wa Afrika hawaridhishwi na demokrasia zao, ingawa kihistoria wamekuwa na ushiriki mdogo wa kisiasa kuliko watu wazima.

Hata hivyo, Gen Z wa Kenya walivunja mtazamo huo, wakithibitisha kuwa vijana wa Afrika hawajakata tamaa kisiasa—wamechoshwa tu na siasa za zamani.