Rais Biya abadili wakuu wa jeshi akilenga kukatalia uongozini
YAOUNDE, CAMEROON
RAIS wa Cameroon Paul Biya, 92, kiongozi mkongwe zaidi duniani, ametekeleza mabadiliko kwenye nyadhifa za juu katika idara ya jeshi katika hali inayoonekana kama kujiandaa kwa vyovyote vile kusalia mamlakani.
Biya ametangaza kuwa atawania urais na hatua hiyo imezua ghadhabu kutoka kwa wengi wa raia wa nchi hiyo ambao wanapinga uamuzi wake.
Mabadiliko hayo yaliyotangazwa Jumatano usiku, yaliathiri karibu idara zote za kijeshi huku akidaiwa kuwaweka wandani wake na kuwaondoa wale anaowatilia shaka.
Idara ya jeshi la wanahewa lilipewa mshikilikizi mpya kwenye uongozi wake pamoja na jeshi la wanamaji huku pia mabrigedia wanane wakipandishwa ngazi hadi kuwa meja jenerali.
Kati ya majenerali waliopandishwa ni mshirikishi wa kikosi cha BIR cha kupambana na ugaidi ambaye anaonekana muhimu zaidi katika ulinzi na usalama wa Biya.
Pia amri ya Biya ilimteua mshauri mpya wa rais kuhusu masuala ya jeshini.
Mabadiliko hayo mapya yalitolewa siku mbili baada ya Biya, ambaye amekuwa mamlakani tangu 1982, kutangaza kuwa atawania muhula wa nane wa urais Cameroon.
Uchaguzi huo utaandaliwa mnamo Oktoba 12. Muhula wa saba akifanikiwa kuupata, utamweka Biya madarakani hadi atinge umri wa miaka 100.
Serikali nayo imesisitiza kuwa Biya yupo kwenye hali nzuri kiafya na kupuuza wasiwasi wowote kuhusu afya yake kuwa hatarini.
Mshauri na mtaalamu wa masuala ya usalama na amani jijini Younde Anthony Antem amesema Biya anaunda kikosi cha jeshi ambacho ni waaminifu kwake ili kuhakikisha anasalia madarakani kwa njia zozote zile.
Mtaalamu mwengine wa usalama Celestin Delanga naye alisema kuna nafasi kubwa Biya atatumia njia zozote zile ili achaguliwe tena ila analenga kuzima maandamano kabla na baada ya kura hiyo ya Oktoba.
Cameroon imekuwa ikiandamwa na utovu wa usalama hasa uhasama na makundi ya kigaidi na vitisho kutoka wapiganaji wa Kiislamu kutoka Nigeria ambao wapo kaskazini mwa Cameroon.