Kitendawili na wasiwasi mgonjwa mwingine akiuawa katika wodi Hospitali Kuu ya Kenyatta
Mgonjwa mwingine aliuawa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Alhamisi, hali inayozua wasiwasi mpya kuhusu usalama wa wagonjwa katika hospitali kubwa zaidi ya rufaa nchini.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka kwa mamlaka husika, mgonjwa wa kiume mwenye alipatikana akiwa amefariki katika kitanda chake katika wodi 7B. Mashahidi walieleza kuwa mgonjwa huyo alikuwa amelowa damu na majeraha mabaya kichwani.
Maafisa wa usalama wakiongozwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) waliitwa hospitalini humo ili kubaini kilichotokea na nani alihusika na kifo cha mgonjwa huyo.
Katika taarifa iliyotolewa saa chache baada ya tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa KNH, William Sigilai, alithibitisha kwamba mnamo Alhamisi, Juni 17, kuwa mgonjwa huyo alipatikana amekufa muda mfupi baada ya saa za wageni kutembelewa kukamilika saa nane mchana.
“Tunasikitika sana kuthibitisha tukio la kifo cha kusikitisha cha mgonjwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta. Mchana wa Julai 17, 2025, saa nane kamili baada ya saa za kuwatembelea wagonjwa, mgonjwa alipatikana katika wodi ya matibabu akiwa amelala kwenye mashuka yaliyolowa damu. Alikaguliwa na kuthibitishwa kuwa amefariki,” alisema Mkurugenzi Mkuu.
“Suala hili limeripotiwa kwa DCI pamoja na vyombo vingine vya usalama vya serikali. Tunatoa pole zetu kwa familia ya marehemu wakati huu mgumu,” aliongeza.
Hospitali hiyo ilitoa pole kwa familia na kuahidi Wakenya kuwa imejizatiti katika kuhakikisha usalama wa wagonjwa, na kwamba itatoa taarifa zaidi kadri uchunguzi unavyoendelea.
Tukio hili ni la pili mwaka huu baada ya mgonjwa kuuawa katika mazingira ya kutatanisha hospitalini humo.
Mnamo Februari, mgonjwa mwingine alipatikana ameuwawa ndani ya hospitali hiyo baada ya kudungwa kisu na mtu asiyejulikana usiku wa Alhamisi, Februari 6.