Ruto atashinda kihalali 2027, asema Mudavadi
Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi jana alikemea viongozi wa kisiasa wanaodai kuwa Rais Ruto atatumia mbinu za udanganyifu kushinda muhula wa pili katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Mudavadi alionya wale wanaotoa matamshi ambayo yanaweza kudhoofisha imani ya umma kwa serikali ya Ruto na kuchochea mvutano wa kisiasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa 2027.
Alihakikishia nchi kuwa Rais Ruto atashinda kwa njia ya kidemokrasia licha ya madai ya baadhi ya wanasiasa wakiwemo wa upande wa serikali kwamba atatumia mbinu zisizo halali kubakia madarakani.
Makamu huyo wa zamani wa Rais alisema kuwa rekodi ya maendeleo ya Ruto itamfanya ashinde kirahisi bila haja ya kutumia njia za udanganyifu.
Akizungumza katika eneo la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega, wakati wa mpango wa kuwawezesha wanawake kiuchumi, Mudavadi alikana uvumi unaoenezwa na baadhi ya wanasiasa wa jamii ya Waluhya kwamba anapanga kujiondoa katika serikali ya Ruto ili kugombea urais mwaka wa 2027.
Ilikuwa wazi kupitia hotuba yake kuwa ataendelea kuwa upande wa Rais Ruto, ambapo alisema Ruto atawashinda wapinzani wake ambao hawana mpangilio wala mshikamano.
“Kuelekea uchaguzi wa 2022, mimi na Wetang’ula tulichambua hali ya kisiasa na tukagundua kuwa William Ruto angeibuka mshindi. Ndiyo sababu tulijiunga naye. Leo ninasimama tena mbele yenu kuwaambia kuwa Ruto atashinda tena 2027. Watu wa jamii yetu wajipange kuunga mkono upande wa ushindi,” alisema Mudavadi.
Alitoa wito kwa Wakenya kuendeleza imani yao kwa taasisi za kitaifa, hasa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambayo hivi majuzi iliundwa upya, akisema kuwa tume hiyo itasimamia uchaguzi huru na wa haki.
“IEBC si ya serikali ya Kenya Kwanza, ni taasisi ya taifa la Kenya. Tusiwe watu wa kuzua shaka kuhusu tume hii. Itasimamia uchaguzi wa haki na wazi. Upinzani unapaswa kuacha kupanda mbegu za uhasama ili walazimike kuleta vurugu,” alisema Mudavadi.
Awali akiwa Malava, Mudavadi aliwaonya viongozi wa Kenya Kwanza dhidi ya kutoa matamshi kama hayo katika mikutano ya hadhara akisema maneno kama hayo huanzisha taharuki ya kisiasa.
“Viongozi wa Kenya Kwanza wanaodai kuwa Ruto ataiba kura waache ujinga huo. Ruto hataiba kura zozote, atashinda uchaguzi kihalali,” alisisitiza.
Naibu Rais Kithure Kindiki naye alitoa wito kwa Wakenya kuunga mkono azma ya Rais Ruto ya kuchaguliwa tena, akitaja miradi mingi ya maendeleo inayoendelea kote nchini kama msingi wa muhula wa pili wa Ruto.
“Serikali ya Kenya Kwanza chini ya uongozi wa Rais Ruto imetekeleza miradi mingi tuliyokuwa tumeahidi kama nyumba nafuu, kilimo, afya, umeme na usambazaji wa maji,” alisema Kindiki.
Alisema kuwa Rais Ruto atashinda uchaguzi wa 2027 kwa haki, huku akiwasihi wapinzani kuacha siasa za matusi.
Alikosoa kauli ya “Ruto lazima aende” akisema haiwezi kuwasaidia wapinzani kushinda uchaguzi.
Aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua amekuwa akimlaumu Rais Ruto kwa kudhibiti uteuzi wa makamishna wa IEBC kwa lengo la kushawishi matokeo ya uchaguzi wa 2027.
Lakini Kindiki alisema kazi ya IEBC ni kuandaa uchaguzi wa kuaminika bila kujali nani yuko madarakani.
Kumekuwa na wasiwasi mkubwa baada ya viongozi walio katika kambi ya Rais kuapa kwamba watahakikisha ushindi wa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027 kwa njia zozote. Mnamo Julai 12, 2025, Mwakilishi wa wanawake wa Wajir Fatuma Abdi Jehow, aliwasha moto kwa kusema kuwa viongozi wa eneo hilo wako tayari kuiba kura ili Rais Ruto ashinde.
“Sisi kama Wabunge wa Kaskazini Mashariki, hatuzungumzi sana. Kuhusu Rais tunasema mihula wawili. Tunangojea kura, hata kama hatuna kura, tutaiba kwa ajili yake. Hilo si siri.”
Mbunge wa Kapsaret, Oscar Sudi, alisema “wanaosema Ruto aondoke wajue hakuna mahali tunakoenda. Hapa hakuna rais aliyewahi kuhudumu miaka mitano tu.”
William Kamket (Tiaty) alinukuliwa akiapa “sisi watu wa Baringo tunajua historia ya miaka 24 ya madaraka. Tuko tayari kusema Rais aendelee” naye Nelson Koech (Belgut) alikosoa upinzani akisema “Kibaki na Uhuru hawakuhudumu muhula mmoja. Tuna akili,” kauli ambazo zilichukuliwa kumaanisha wanaweza kutumia mbinu za kuiba kura Rais Ruto ashinde muhula wa pili.