Makala

Msimamizi wa mali ya marehemu lazima afuate masharti ya wosia kikamilifu

Na BENSON MATHEKA July 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Sheria ya Urithi ni msingi mkuu wa jinsi mali ya mtu inavyogawanywa baada ya kifo chake, iwe aliandika wosia au la. Sheria hii inalenga kuhakikisha kuwa mali ya marehemu inasimamiwa kwa njia ya haki, uwazi na kwa kuzingatia matakwa ya marehemu pamoja na haki za wanafamilia wake.

Kwa mujibu wa Sheria ya Urithi, wosia halali ni lazima uandikwe kwa maandishi, usainiwe na mtoa wosia mwenyewe, na ushuhudiwe na watu wawili au zaidi. Aidha, mtoa wosia lazima awe na akili timamu na asiwe amelazimishwa kuandika wosia huo.

Katika kesi ya Karanja dhidi ya Karanja iliyoamuliwa 2019 mahakama ilitilia mkazo umuhimu wa kufuata masharti ya sheria katika kutekeleza wosia, na kumtaka msimamizi wa mali kufuata matakwa ya marehemu.

Iwapo kuna wosia, familia inapaswa kuwasilisha mahakamani ombi la kuthibitishwa kwa wosia huo, ambapo msimamizi atateuliwa rasmi. Msimamizi huyu hushughulikia madeni, ushuru, na hatimaye kugawa mali kwa walengwa kama ilivyoelekezwa kwenye wosia.

Sheria hii inatambua haki za mwenzi aliyebaki hai ambaye hupewa sehemu maalum ya mali(nilifafanua katika Makala ya wiki jana.soma hapa https://taifaleo.nation.co.ke/makala/pambo/mwongozo-wa-urithi-wa-mali-ya-marehemu-asipoacha-wosia/), watoto wote bila kujali jinsia, umri au hali ya ndoa, wanapewa mgao sawa wa mali na watu wengine ambao walikuwa wakimtegemea marehemu kifedha.

Hili linalenga kuondoa ubaguzi unaotokana na mila au mitazamo ya kijinsia, ambayo kwa muda mrefu imewadhulumu baadhi ya warithi halali.

Katika hali ambapo mtu amefariki bila kuacha wosia, sheria inaelekeza kuwa mahakama itamteua msimamizi wa mali. Kipaumbele hutolewa kwa mjane wa marehemu, watoto, au jamaa wa karibu zaidi.

Msimamizi huyu husimamia mchakato wa kuthamini mali, kulipa madeni, na kugawa kilichobaki kwa warithi kwa mujibu wa sheria.

Kenya ni taifa lenye jamii nyingi zinazofuata mila tofauti kuhusu urithi. Sheria ya Urithi inatambua mila hizi, lakini panapozuka migongano baina ya sheria na desturi, sheria ndio hutumiwa.

Katika uamuzi wa kesi ya Mbugua dhidi ya Mbugua mwaka wa 2015 mahakama ilieleza kuwa mila zinaweza kuzingatiwa ilmradi hazikinzani na kanuni za usawa na haki zilizo katika Sheria ya Urithi.

Kwa jumla, Sheria ya Urithi inalenga kuleta usawa na utaratibu katika ugawaji wa mali ya marehemu. Iwapo jamii itaielewa na kuiheshimu, migogoro ya kifamilia kuhusu urithi itapungua pakubwa.

Ni wajibu wa kila mmoja kujua haki zake, kuandika wosia mapema, na kuhakikisha kuwa mali yake itasimamiwa kwa njia ya haki atakapoaga dunia.