Habari

Natembeya: Vikwazo vimeisha, narudi ofisini Jumatatu

Na EVANS JAOLA July 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Trans Nzoia George Natembeya anatarajiwa kuanza kufanya kazi katika afisi zake rasmi Jumatatu, Julai 21, 2025 baada ya marufuku aliyowekewa kukamilika.

Kwenye taarifa katika mitandao yake ya kijamii, Gavana Natembeya anasema atawasili katika majengo ya afisi zake kesho Jumatatu kwa kuwa marufuku ya siku 60 aliyowekewa na Mahakama ya Kukabili kesi za Ufisadi ishaisha.

“Amri ya mahakama ilituzuia kuingia kwenye majengo ya afisi zetu zilizoko Town Hall kwa kipindi cha siku 60, jambo ambalo tuliheshimu kwa uadilifu na utiifu mkubwa kwa sheria. Kipindi hicho sasa kimeisha kwa hivyo tunarejea kazini Jumatatu si kukalia afisi tu bali kutumikia wananchi wa Kaunti ya Trans Nzoia kwa kujitolea kukubwa,” ikasema taarifa yake.

Baadhi ya wakazi wa kaunti hiyo wameelezea kufurahishwa na hatua hiyo huku wakiionya serikali kuu dhidi ya kutumia asasi zake kuhangaisha watu ambao hawakubaliani nao kimaoni.