Siondoki serikali ya Ruto kwa sasa ingawa nampima tu hadi 2027 – Raila
KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, amepuuza uwezekano wa kujiondoa mapema katika serikali Jumuishi inayoongozwa na Rais William Ruto, akisema ataendelea kushirikiana na Rais hadi mwaka wa 2027.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema ataendelea kufanya kazi na Rais Ruto chini ya muundo wa serikali Jumuishi hadi 2027, akisema hatashiriki katika mazungumzo ya urithi kabla ya muda, hadi serikali ya Kenya Kwanza itimize muhula wake.
Lakini alitoa pendekezo la kushangaza kuhusu uchaguzi ambalo linaweza kuzua gumzo kote nchini, akipendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa uchaguzi wa Kenya, ikiwa ni pamoja na kuondoa kabisa rejista ya sasa ya wapigakura na wito wa kishujaa wa kuwawezesha Wakenya kupiga kura kwa kutumia tu vitambulisho vyao vya taifa.
Amehimiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyoundwa hivi karibuni kuchukua hatua za haraka na kusafisha rejista, ili kurejesha imani ya umma katika uchaguzi ujao.
Katika mahojiano maalum na NTV na Taifa Leo katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi, Jumamosi, Bw Odinga, ambaye amewania urais mara tano, alisema nchi bado inakabiliwa na mzozo wa kitaifa na kwamba uamuzi wa ODM kushirikiana na utawala wa Rais Ruto ulifanywa kwa maslahi ya utulivu wa taifa.
“Tumeweka bayana kuwa tuko katika Serikali Jumuishi hadi 2027. Hatukusema tutafanya kazi na UDA baada ya 2027. Haya ni mambo tutakayojadili kwa wakati muafaka na uamuzi ufanywe na wanachama wa ODM, si Raila Odinga pekee,” alisema kiongozi huyo.
Alitaja ushirikiano wa sasa kuwa jibu kwa maandamano ya mwaka jana yaliyoendeshwa na vijana, ambayo nusura yatumbukize taifa katika vita vya kiraia.
Kiongozi huyo wa ODM alifichua kuwa kama asingechukua hatua kwa wakati, Kenya ingekuwa hatarini kutumbukia katika hali kama ile ya Somalia, Haiti au Sudan.
“Mwaka wa 2023 tulikuwa barabarani tukilalamika kuhusu masuala muhimu kama haki ya uchaguzi, gharama za maisha na ufisadi katika serikali. Serikali ilitumia nguvu na ukatili dhidi yetu. Tulipoteza watu wapatao 70. Na tulipotaka kuwatambua, hakuna jaji aliyeturuhusu. Mwishowe tulifanya hivyo kwa siri,” alisema Bw Odinga.
Alibainisha kuwa maandamano yao, yaliyofuatiwa na ya Gen Z mwezi Juni 2024, yaliweka wazi mianya mikubwa katika utawala wa nchi, na kusababisha jamii ya kimataifa kuingilia kati, na kupendekeza Rais wa Tanzania Samia Suluhu na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo kupatanisha mirengo iliyokuwa ikipigana.
Mdahalo huo ulisababisha kuundwa kwa Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO), ambayo ripoti yake iliwasilishwa bungeni.
“Kama ripoti ya NADCO ingetekelezwa mapema, maandamano ya Gen Z yasingetokea. Vijana walienda mbali zaidi kuliko tulivyofika sisi. Walishambulia Bunge, Mahakama na walipanga kuenda Ikulu kabla ya kuzuiwa,” alisema Bw Odinga.
Alifafanua kuwa wakati ghadhabu na vitisho vya mapinduzi ya jeshi vilipoongezeka, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa Amerika wakati huo, alimshauri kuanzisha mazungumzo na Rais Ruto kwa ajili ya amani nchini.
“Ingawa awali nilikataa kuzungumza na Ruto, hali ya taifa ilinilazimu,” alifichua.
Bw Odinga alisema uamuzi wa kuwaruhusu wanachama wa ODM kujiunga na serikali uliafikiwa baada ya mashauriano ndani ya chama na viongozi wa Azimio.
“Mwanzoni nilikuwa sipendi hilo. Lakini wenzangu ndani ya chama walihisi tulihitaji kusaidia kuimarisha nchi. Hivyo, tuliwaruhusu wataalamu wetu kujiunga na serikali. Hata hivyo, ODM kama chama hakikujiunga rasmi na serikali. Hilo linaweza kutokea baada ya mazungumzo rasmi kulingana na ajenda ya wazi na hilo lilichangia makubaliano ya hoja 10.”
Bw Odinga alisisitiza kuwa mojawapo ya ajenda 10 ni kutekelezwa kwa ripoti ya NADCO na kwamba chama kimeunda kikosi cha ndani kutathmini utekelezaji wake.
Alionya kuwa iwapo masuala muhimu hayatatatuliwa, ODM haitasita kukatiza ushirikiano na UDA. “Kuna mstari hatari ambao ukivukwa, tutafanya uamuzi.
Kwa sasa, baadhi ya masuala yametimizwa ila mengine bado. Tutafanya tathmini na kuamua kwa niaba ya chama,” alisema.
Akijibu wakosoaji wanaomtuhumu kwa kulegeza msimamo wake wa upinzani, Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema uamuzi wake wa kuunga mkono mazungumzo umetokana na uzalendo kwa taifa.
“Sijali kuhusu wale wasioelewa kile ninachojaribu kufanya. Ninajaribu kuwashawishi waone mambo kutoka kwa mtazamo wangu. Wajibu wa kuwa Raila Odinga ni kubwa, lakini siku zote nimetanguliza maslahi ya nchi,” alisema.
Kuhusu azma yake ya kugombea urais 2027, Bw Odinga alisema bado hajafanya uamuzi na akatahadharisha kuwa ni mapema mno kuanza kuzungumzia uchaguzi ujao.
“Sijasema kwamba nitagombea. Si lazima nigombee. Naweza kumuunga mkono mtu mwingine, lakini pia naweza kugombea nikitaka. Kwa sasa, nimejikita katika kuimarisha ODM,” alisema.
Alipoulizwa ikiwa atamuunga mkono kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, ambaye amemuunga mkono katika chaguzi tatu zilizopita – mara mbili kama mgombea mwenza wake mwaka 2013 na 2017 — Bw Odinga alisema:
“Mimi na Steve ni marafiki. Ninamheshimu sana. Lakini hajaniomba msaada wangu. Wakati ukifika, tutaketi chini na kutathmini ni nani aliye na nafasi bora ya kubeba bendera. Lakini haitakuwa uamuzi wangu pekee — chama ndicho kitaamua mwelekeo tutakaochukua.”
Alipuuzilia mbali ripoti kwamba anaweza kuwa anafikiria tiketi ya pamoja ya Ruto-Kalonzo kama “upuuzi mtupu” na akasisitiza kwamba mwelekeo wowote wa kisiasa wa baadaye utakuja tu baada ya mashauriano ya kina.
Kuhusu tuhuma za kutetereka kwa misimamo yake kwa kushirikiana na wale aliowapinga awali, Bw Odinga alitetea historia yake kama mtetezi wa demokrasia.
“Nimekuwa nikisimama daima kwa ajili ya ukweli na haki. Tulijitokeza wazi tukidai mabadiliko, na maisha mengi yalipotea katika mchakato huo. Hatukukubali maovu — tulichukua hatua kwa ajili ya amani,” alisema.
Alisisitiza kuwa anapinga matumizi ya hatua zisizo halali dhidi ya waandamanaji, ikiwemo matumizi ya nguvu mwaka jana na maagizo kutoka kwa maafisa wa serikali ya kuwapiga risasi waandamanaji.
Bw Odinga alisema suala la kuwalipa fidia waathiriwa wa ukatili wa polisi bado liko mezani, na jopokazi limeundwa kusimamia mchakato huo.
“Kuna hazina ya dharura katika bajeti ya kitaifa. Malipo ya fidia yatafanyika hivi karibuni. Kuna jopokazi linaloshughulikia suala hilo,” alisema.