Mwanafunzi wa Kakamega High afa uwanjani akisakata soka
MSIBA umekumba Shule ya Upili ya Wavulana ya Kakamega baada ya mwanafunzi wa kidato cha tatu kuaga dunia ghafla wakati wa mashindano ya soka baina ya darasa mjini Kakamega.
David Owino Oduor, 16, alikuwa akicheza soka katika mashindano hayo mnamo Julai 20, 2025, aliporuka na kupiga kwa kichwa mpira wa juu uliojaa wavuni, lakini alianguka baada ya kurejea chini na kupoteza fahamu.
Mkuu wa shule hiyo, Dkt Julius Mambili, amesema kuwa kijana huyo alikimbizwa katika zahanati ya shule kwa huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega, ambako alithibitishwa kufariki alipowasili.
“Alifariki kutokana na hali ya kiasili, lakini tunasubiri ripoti ya upasuaji wa maiti kutoka hospitalini ili kubaini chanzo halisi cha kifo chake,” akasema Dkt Mambili.
Kifo cha ghafla cha Oduor, ambaye alikuwa ameiongoza timu ya darasa la 3B kwa kufunga mabao mawili kabla ya tukio hilo, kimewaacha wanafunzi, walimu, wazazi na jamii ya elimu katika Kaunti ya Kakamega wakiwa na huzuni na mshtuko mkubwa.
“Hakuwa na historia ya matatizo ya kiafya na alikuwa miongoni mwa wanafunzi bora kitaaluma darasani. Alikuwa na ushirikiano mzuri na wenzake na alikuwa na nidhamu ya hali ya juu kwa walimu wake. Hii ni hasara kubwa siyo kwa wazazi wake, tu bali pia kwa shule,” akaomboleza Dkt Mambili.
Msimamizi Mkuu wa Kitengo cha Afya katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega, Dkt Christian Lamba, alisema wamepokea mwili wa mwanafunzi huyo na wanasubiri wazazi wake waidhinishe kufanyika kwa upasuaji wa maiti ili kubaini chanzo cha kifo.
“Tutaweza kujua kilichosababisha kifo baada ya kufanyika kwa upasuaji wa maiti. Kwa sasa chanzo hakijafahamika, lakini tunawapa pole familia na shule nzima,” akasema Dkt Lamba.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kakamega Kati, Vincent Cherutich, alifichua kuwa uchunguzi kuhusu kifo hicho tayari umeanzishwa.
“Tulipokea simu kutoka kwa mkuu wa shule akitufahamisha kuwa mwanafunzi mmoja alikuwa amezimia na kufariki wakati wa mechi ya soka ya madarasa. Tulipofika shuleni tulibaini kuwa alikuwa tayari amekimbizwa katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega ambako alithibitishwa kuwa amefariki. Tumeshafungua uchunguzi kuhusu kifo hicho,” alisema Cherutich.
Aliongeza kuwa uchunguzi huo utabaini kama kifo hicho kilitokana na sababu za kawaida au ikiwa kulikuwa na hila.
“Uchunguzi utaonyesha kama mwanafunzi alikufa kwa sababu za kawaida au kulikuwa na njama yoyote,” akasema.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Kaunti ya Kakamega, ambako upasuaji wa maiti unatarajiwa kufanyika.
-Imetafsiriwa na Geoffrey Anene