Polisi Turkana walilia Murkomen hawana mafuta ya magari
SHUGHULI za usalama katika Kaunti ya Turkana zimelemazwa na ukosefu wa mafuta polisi wakimtaka Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen aangazie suala hilo ili wachape kazi bila changamoto nyingi.
Wakiwasilisha malalamishi yao kwa waziri huyo, wakuu wa usalama walisema wamelazimika kuenda hadi Kitale kuyaweka magari yao mafuta baada ya bidhaa hiyo muhimu kukosekana Turkana.
Polisi ambao wanahudumu katika kituo cha polisi cha Kibich kilichoko mpakani, hulazimika kuenda hadi Kitale hali hiyo ikitia doa juhudi za kuhakikisha usalama.
Mkuu wa Polisi wa Turkana Kusini William Adenyo, aliambia Bw Murkomen kuwa mafuta huwaishia ndani ya siku 15 tu kutokana na kilomita nyingi wanazosafiri.
Bw Adenyo alisema kuwa vituo vingi pia havina magari yaliyoko katika hali sawa, mengine yakiwa makukuu na hali huwa mbaya zaidi kama hamna mafuta.
“Katika eneo la Turkana Kusini tangu maafisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) wavamiwe na polisi wanne wauawe kati ya Kainuk na Lokichar ambapo magari manne pia yalichomwa, hatujawahi kuyapata magari mengine na tuna machache sana,” akasema Bw Adenyo.
“Tunategemea magari hayo machache kuendeleza oparesheni na shughuli zetu nyingine za usalama. Tunawasafirisha mabusu kutoka Kainuk hadi Lodwar wafike kortini umbali wa kilomita 167,” akaongeza.
Afisa huyo pia alilalamika uchache wa polisi Turkana akisema wengi wanaotumwa huku huwafiki na wale wanaohamishwa huwa nafasi zao hazijazwi.
Alisema kuwa ukosefu wa mafuta pia yamechangia maafisa wa usalama kujipata katika hali mbaya hasa wanapovamiwa na magaidi.