Hofu takwimu zikionyesha wanawake zaidi hawanyonyeshi watoto
AKINA mama watatu kati ya 10 Kenya hawanyonyeshi watoto wao bali wanategemea lishe mbadala, kulingana na data ya hivi punde kutoka kwa Wizara ya Afya.
Idara ya Afya ya Umma katika wizara hiyo inaripoti kwamba mtindo wa akina mama wenye watoto wachanga kuwalisha wanao kwa njia ya matumizi ya chupa, umeongezeka kwa kiwango cha asilimia 12; kutoka asilimia 22 mnamo 2022 hadi asilimia 34 mwaka huu wa 2025.
Mwenendo huu unaotisha, kulingana na Katibu wa Idara ya Afya ya Umma Mary Muthoni, umeshamiri zaidi miongoni mwa tabaka la wanawake walioajiriwa na ambao hawana wakati wa kuwanyonyesha watoto wao.
Hii ni kutokana na hali ya wao kubanwa na shughuli za kikazi na presha kutoka kwa wasimamizi wao wanaowashurutisha kuzipa kipaumbele kazi zao badala ya majukumu yao ya uzazi.
Pia, katibu huyo alisema waajiri wamefeli kutoa mazingira faafu kwa wafanyakazi wao kunyonyesha wanao wakiwa kazini
“Unyonyeshaji unapasa kuwa mojawapo ya furaha ya mama mzazi. Ndio wakati wa kipekee ambapo mama anatagusana na mwanawe na maziwa ya matiti ya mama ni muhimu katika kuzuia magonjwa na maambukizi yanayoweza kumwathiri mtoto. Maziwa ya mama humsaidia mtoto kujenga kinga ya mwili wake,” Katibu huyo wa Wizara akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano.
Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (UNICEF) linakubaliana na msimamo wa Wizara ya Afya kwa kuhimiza unyonyeshaji wa watoto.
Aidha, shirika hilo linatoa mwongozo kuhusu njia salama za mtindo wa watoto wapewe lishe mbadala kwa chupa endapo mama hataweza kumnyonyesha mwanawe.
Unicef inasisitiza umuhimu wa uwepo wa ratiba ya kulishwa kwa watoto, ukaribu na watoto wanapopewa lishe na kuanzishwa kwa aina mbadala ya chakula inapohitajika.
“Kuanzia mtoto anapozaliwa hadi anapotimu miezi sita, anafaa kulishwa kwa maziwa ya matiti pekee wala siyo aina nyingine ya lishe. Maziwa ya mama huwa salama na yanasheheni madini na virutubisho vyote ambavyo mtoto anahitaji. Isitoshe, maziwa ya mama ni safi na salama na rahisi kupatikana,” inasema ripoti ya Unicef kuhusu Unyonyeshaji Duniani, 2025.
-IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA