Mzee kugawana pensheni na ex baada ya kuruka malezi
Mzee mstaafu amejipata pabaya baada ya Mahakama Kuu kukataa kusitisha utekelezaji wa amri inayomtaka kugawana pensheni yake ya uzeeni na mpenzi wake wa zamani ili kugharamia mahitaji ya watoto wao.
Mahakama hiyo pia iliunga mkono uamuzi wa hakimu wa mahakama ya watoto uliomwelekeza mwajiri wa zamani wa mstaafu huyo kulipa deni la matunzo ya watoto linalofikia Sh178,790 kutoka kwa pensheni yake.
Mzee huyo, aliyejulikana kwa kifupi kama Bw MST, aliacha kulipa matunzo mwaka jana baada ya kuugua maradhi ya mfumo wa neva ambayo, kulingana naye, yanahitaji matibabu ya gharama kubwa. Alisema aliomba mkopo kufadhili matibabu hayo.
Mbali na deni hilo, mahakama ya watoto pia iliagiza mwajiri wake wa zamani kuachilia thuluthi moja ya pensheni yake kwa mpenzi wake wa zamani, Bi LNK, ili kufadhili masomo ya watoto.
Bw MST alikuwa ameomba Mahakama Kuu isimamishe utekelezaji wa amri hiyo akidai hakimu hakuzingatia kuwa wazazi wote wawili wana jukumu la kushiriki katika malezi ya watoto kwa usawa. Alisema Bi LNK hajawahi kuonyesha mchango wake wa kifedha na anambebesha mzigo wote wa gharama.
Alisema kuwa kwa sasa anaishi kwa pensheni pekee ambayo sehemu kubwa hutumika kulipa mkopo wa matibabu. Hali hiyo ilisababisha akose kulipa matunzo ya watoto kwa wakati.
Bi LNK aliwasilisha ombi mahakamani la kutaka deni hilo lishughulikiwe kupitia kukatwa kwa sehemu ya pensheni ya Bw MST, na ndipo mahakama ikatoa uamuzi huo mnamo Januari 25, 2025.
Bw MST alisema utekelezaji wa agizo hilo utamletea madhara makubwa kwani pensheni ndiyo chanzo chake pekee cha mapato.
Aliongeza kuwa asilimia 30 ya pensheni yake ya kila mwezi — takriban Sh30,000 — tayari hukatwa na kutumwa moja kwa moja kwa akaunti ya Bi LNK kwa ajili ya masomo na mahitaji ya watoto. Bi LNK alithibitisha hilo mahakamani, huku Bw MST akisema ana watu wengine wanaomtegemea pia.
Hata hivyo, Jaji Helene Namisi alitupilia mbali ombi lake akisisitiza kuwa maslahi ya watoto ndiyo muhimu zaidi.
“Ingawa mlalamishi ameonyesha kuwa ana hoja ya kukata rufaa, sijaona sababu ya kuridhika kwamba kusitisha utekelezaji wa agizo hilo kutakuwa kwa maslahi ya watoto. Nimebaini kuwa hakuna msingi wa kusitisha agizo lililotolewa Januari 25, 2025, kwani kufanya hivyo kutakuwa na madhara kwa ustawi wa watoto,” alisema jaji.
“Ninaona ombi hili halina mashiko. Linatupiliwa mbali kikamilifu. Kwa hivyo, agizo la Januari 25, 2025 lililotolewa na Mahakama ya Watoto, linaendelea kuwa halali na linatekelezeka.”
Bi LNK alipinga vikali ombi hilo akimshutumu Bw MST kwa kukaidi maagizo ya mahakama.
Alisema amebaki peke yake akihudumia watoto kwa mahitaji ya masomo, chakula na afya. Alibainisha kuwa mmoja wa watoto ana hali ya kiafya inayohitaji ukaguzi wa mara kwa mara, jambo ambalo Bw MST amekataa kusaidia.
Bi LNK pia alitilia shaka madai ya Bw.MST kuwa alikopa mkopo wa matibabu, akisema huenda ilikuwa mbinu ya kukwepa majukumu yake kifedha kwani hakuwasilisha ushahidi wowote mahakamani kuthibitisha mkopo huo.
Kuhusu pendekezo la Bw MST la kuweka fedha hizo kwenye akaunti ya pamoja hadi rufaa isikilizwe, Bi LNK alipinga wazo hilo akisema mawasiliano kati yao si mazuri tena.
Alidai kuwa mke wa Bw MST amekuwa akimnyanyasa na kumtukana, hali inayofanya ushirikiano kuwa mgumu.