Ripoti yasema asilimia 30 ya wanafunzi wa Gredi 6 hawawezi kusoma vitabu vya Gredi 3
ASILIMIA 30 ya wanafunzi wa Gredi ya Sita wanaosomea katika shule za umma nchini hawawezi kusoma kitabu cha Kiingereza cha kiwango cha Gredi 3, kulingana na ripoti moja iliyotolewa juzi.
Kulingana na ripoti hiyo ya utafiti kuhusu Hali ya Elimu nchini Kenya iliyotolewa na Wakfu wa Zizi Afrique na Shirika la Usawa Agenda, ni asilimia 40 pekee ya wanafunzi wa Gredi 4 wanaoweza kusoma.
Aidha, ripoti hiyo inaeleza kuwa wanafunzi katika maeneo ya mashambani na maeneo kame ndio waathiriwa wakubwa.
Kwa mfano, wanafunzi wawili kati ya wanafunzi 10 wa Gredi 4 Kaskazini Mashariki mwa Kenya ndio wanaweza kusoma na kuelewa hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha Gredi 3, tofauti na wenzao wanaosomea shule za mijini.
“Viwango vya masomo viko chini zaidi. Ni wanafunzi wanne pekee wa Gredi ya 4 wanaweza kusoma na kuelewa hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha Gredi 3; wanafunzi 3 kati ya 10 wa Gredi 6 hawangeweza kusoma na kuelewa hadhi ya Kiingereza ya kiwango cha Gredi 3,” ripoti inasema.
Inaongeza, “Wanafunzi katika maeneo kame na ya mashambani ndio waathiriwa zaidi kuliko wenzao wanaosomea katika maeneo ya mijini. Katika eneo la Kaskazini Mashariki ni wanafunzi wawili pekee wa Gredi 4 wanaweza kusoma na kuelewa hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha Gredi 3.”
Hii ina maana kuwa maelfu ya wanafunzi wanapanda ngazi katika mfumo wa elimu bila kupata uwezo hitajika wa kusoma kwa manufaa yao katika elimu ya juu na wakiwa watu wazima.
Ripoti hiyo inahusisha hali ya wanafunzi kutoweza kusoma vizuri na udhaifu katika masomo ya chekechea.Kulingana na ripoti hiyo, idadi kubwa ya wanafunzi wenye matatizo ya kusoma, ni wale waliojiunga na shule za msingi kabla ya kusomea shule za chekechea.
Ripoti hiyo inasema kuwa watoto waliosomea katika shule za chekechea wanaweza kufanya vizuri katika somo la Hisabati na somo la Kiingereza ikilinganishwa na wenzao ambao hawahudhuri shule za chekechea.
“Watoto waliohudhuria shule za chekechea kabla ya kujiunga na shule za msingi wako na uwezekano wa asilimia tisa wa kufanya vizuri katika hisabati na asilimia 18 ya wanafunzi katika somo la Kiingereza kuliko wale ambao hawakuhudhuria shule za chekechea,” ripoti hiyo inaeleza.
Licha ya hayo, idadi ya watoto wanaopata nafasi ya masomo ya shule za chekechea ni ndogo katika maeneo mengine ya nchi.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kitaifa, asilimia 7.4 ya watoto waliosajiliwa katika Gredi 1 hawakuwa wamepata nafasi ya kuhudhuria shule za chekechea.
Katika maeneo ya mashambani asilimia 8.4 ya wanafunzi waliojiunga na Gredi 1 hawakupata nafasi ya kuhudhuria shule za chekechea.
Na katika maeneo ya mijini, ni asilimia 6.2 ya wanafunzi wa Gredi 1 hawakuhudhuria shule za chekechea.