Mahakama yazuia Samidoh kukamatwa akisema amestaafu mapema
MAHAKAMA Kuu imempa mwanamuziki wa mitindo ya Mugithi, Samuel Muchoki, almaarufu Samidoh, dhamana ya Sh200,000 kuzuia kukamatwa kwa tuhuma za kutelekeza majukumu yake kama afisa wa polisi.
Agizo la mahakama linajiri huku Samidoh akifichua kuwa tayari amewasilisha, kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) barua ya kustaafu mapema. Aidha, amehusisha tuhuma dhidi yake, kwamba ametelekeza kazi, na kauli zake za kisiasa kuhusu utawala wa Kenya Kwanza.
Jaji Diana Kavedza alisema mahakama iliridhika kuwa uhuru wa Samidoh unatishiwa baada ya NPS kutoa ilani ya kukamatwa kwake mwezi jana. Ilani hiyo ilitolewa siku chache baada ya NPS kuidhinisha safari yake kwenda Amerika. Bw Samidoh, ambaye anahudumu katika Kitengo cha Polisi wa Kupambana na Wezi wa Mifugo (ASTPU), awasilisha ombi la dhamana akiwa ana hofu kwamba angekamatwa akirejea Kenya.
Aliambia mahakama kwamba mpango wa kumkamata “unahusishwa na kauli zangu za kisiasa na ukosoaji wangu wa serikali.”
Alituhumiwa kufeli kufika katika kituo chake cha kazi, Gilgil, kaunti ya Nakuru tangu Mei 27, 2025.
“Mahakama imeridhika kuwa kuna tishio kwa uhuru wa mlalamishi. Kwa hivyo, bila kinga, mlalamishi anaweza kukamatwa na kuzuiliwa kinyume na Katiba,” akasema Jaji Kavedza katika Mahakama ya Kibera.
Jaji huyo pia alimwamuru Samidoh kuwasilisha paspoti yake mahakamani.
Hata hivyo, Jaji Kavedza alifafanua kuwa NPS na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Igonga wako huru kumchunguza na kumshtaki Samidoh kwa uhalifu wowote ule.