Wadau wa elimu wakasirishwa na kupunguzwa kwa mgao wa elimu
Wadau wa elimu wamekasirika vikali baada ya serikali kutangaza kuwa haiwezi kufadhili kikamilifu mpango wa elimu bila malipo, wakionya kuwa sekta ya elimu ya msingi nchini iko katika hatari kubwa kufuatia kupunguzwa kwa mgao wa serikali kwa wanafunzi.
Katika hotuba yake mbele ya Kamati ya Elimu ya Bunge la Taifa, Waziri wa Fedha John Mbadi alikiri kuwa serikali haina uwezo wa kugharamia kwa ukamilifu mipango ya Elimu ya Msingi Bila Malipo (FPE) na Elimu ya Sekondari Bila Malipo (FDSE).
Chini ya mpango wa FPE, kila mwanafunzi anatakiwa kupata Sh1,420 kwa mwaka, wale wa Sekondari Msingi Sh15,042, na wanafunzi wa sekondari Sh22,244.
Hata hivyo, Bw Mbadi alifichua kuwa mgao kwa wanafunzi wa sekondari umepunguzwa kutoka Sh22,244 hadi Sh16,428 kwa mwaka, na kusababisha pengo la Sh5,340 kwa kila mwanafunzi.
Hii imewaacha wakuu wa shule wakikabiliwa na madeni kwa wasambazaji wa bidhaa na mishahara ya wafanyakazi wasio walimu. Hatua hiyo imezua hofu ya ongezeko la wanafunzi wanaoacha shule na mwisho wa sera ya elimu ya msingi bila malipo.
Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari (KESSHA) kimeitaka serikali kuruhusu wazazi kugharamia elimu, kutokana na kupungua kwa mgao huo wa serikali.
“Mkuu wa shule anatarajiwa kuendesha shule bila pesa za kutosha huku akizuiwa kushirikiana na wazazi kuziba pengo la kifedha. Hali hii haiwezi kudumu,” alisema mwenyekiti wa KESSHA, Bw Willy Kuria.
Pia alitaka serikali itoe ruzuku ya dharura kufidia upungufu uliopo kwani shule zilifanya maamuzi ya kifedha kwa msingi wa ahadi ya kupata mgao kamili.
“Hata wakati mgao ulikuwa Sh22,244, bado haukutosha kwani kiwango hicho kilitekelezwa zaidi ya miaka minane iliyopita bila kuzingatia mfumuko wa bei na gharama zilizoongezeka. Thamani halisi ya kiasi hicho imepungua sana, na kufanya iwe vigumu kutoa elimu bora katika mazingira ya sasa,” aliongeza Bw Kuria.
Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA) kilionya kuwa kupunguzwa kwa ufadhili kunaweza kusababisha janga jipya katika sekta ya elimu, na kuwalazimu maelfu ya wanafunzi kuacha shule.
“Hii ni habari ya kushtua kwa wazazi. Wakati huu ambapo wengi bado wanapambana na kupoteza ajira na kupungua kwa mapato, serikali ilipaswa kuongeza mgao, si kuupunguza,” alisema mwenyekiti wa NPA, Bw Silas Obuhatsa.
Chama cha Wadau wa Elimu Kenya (ESAK) kilitoa wito kwa serikali kuitisha mkutano wa kitaifa wa dharura kujadili changamoto ya ufadhili wa shule.
Katibu wa ESAK, Ndung’u Wangenye, alionya kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, elimu ya mamilioni ya watoto iko hatarini.Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari (KUPPET), Akelo Misori, alikashifu serikali kwa kushindwa kushughulikia pengo la fedha katika elimu ya sekondari na kuonya dhidi ya kuhamisha mzigo huo kwa wazazi waliolemewa tayari.
Hata hivyo, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alipinga madai kuwa serikali imefuta sera ya elimu bila malipo, akisema kuwa wamepunguza kiasi cha mgao kutokana na changamoto za bajeti pekee.