Habari za Kitaifa

Agizo la Rais ‘piga risasi mguuni’ sasa latua kortini

Na  JOSEPH WANGUI July 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANASHERIA Mkuu Dorcas Oduor anatarajiwa kumtetea Rais William Ruto mahakamani kufuatia agizo lake kwa maafisa wa polisi kuhusu matumizi ya nguvu kali dhidi ya waandamanaji wanaozua fujo.

Kesi hiyo, iliyowasilishwa na mwanaharakati wa haki za binadamu Dunstan Riziki Makokha, inahusu agizo la Rais la “piga risasi mguuni” kwa maafisa wa usalama, alilotoa kukabili maandamano ya vijana wa Gen Z dhidi ya serikali.

Kesi hiyo pia inahusisha agizo la Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kwa polisi “kuua kwa kupiga risasi” waandamanaji.Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja tayari amewasilisha majibu yake mahakamani akikana kupokea maagizo kama hayo kutoka kwa Rais au Waziri Murkomen.

Anasema maafisa wa polisi wanawajibika binafsi kwa matumizi ya silaha na kwamba kila wakati wanapaswa kutii tu maagizo yaliyo halali.“Maombi yanayotakiwa hayadhihirishi ukiukaji wowote wa haki za kikatiba; yamejengwa juu ya dhana zisizo na msingi, na yanapaswa kutupiliwa mbali kwa sababu hayakidhi mahitaji ya kisheria,” alisema Bw Kanja kupitia kwa wakili wa serikali, Bw Peter Muriithi akiwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Bw Kanja, matumizi ya nguvu au silaha na polisi yamekitwa katika kanuni na sheria, na ni juu ya afisa binafsi wa polisi kuamua lini anapaswa kutumia risasi kulingana na hali halisi.

Mwanasheria Mkuu bado hajawasilisha majibu kwa niaba ya Rais.

“Mshtakiwa wa pili (Inspekta Jenerali) anaweza kupokea maagizo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma tu kuhusiana na uchunguzi wa madai ya makosa ya jinai, ilhali Waziri wa Usalama anatoa mwelekeo wa kisera tu na kwa maandishi, kulingana na Kifungu cha 245(5) cha Katiba ya Kenya. Mshtakiwa wa pili anakana vikali kupokea maagizo yoyote yanayohusiana na kiini cha kesi hii, na mlalamishi anatakiwa kuthibitisha madai hayo kwa ushahidi wa kina,” Bw Kanja alisema.

Wakili Makokha anasema kwamba kutokana na maagizo yaliyotolewa na Rais na Waziri kwa polisi, maafisa wa usalama wako katika hatari ya kugeuka kuwa wahuni kwa kupuuza sheria kiholela, hali inayotishia usalama wa taifa, uhuru wa kutembea na haki ya kukusanyika na kuandamana.

“Maagizo haya ni ruhusa haramu kwa polisi kujipa mamlaka ya kuwa washtaki, wachunguzi, waendesha mashtaka, majaji na watekelezaji wa sheria kwa wakati mmoja – jambo linalohatarisha taifa. Agizo hilo linapokonya haki ya kuishi na linafungua mlango kwa mauaji ya kiholela,” alisema Bw Makokha.

Anaamini utekelezaji wa maagizo hayo utasababisha Wakenya wengi zaidi kupoteza maisha kwa sababu ya ukatili wa polisi na matumizi mabaya ya mamlaka “kwa misingi ya maagizo kutoka kwa waliopewa mamlaka ya kisiasa, kisheria na kisera kuhusiana na operesheni za polisi.”

“Maagizo ya ‘piga risasi kuua’ na ‘piga risasi mguuni’ yatashusha hadhi ya Kenya katika rekodi ya haki za binadamu na kuiweka kwenye hatari ya kukemewa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa. Maagizo haya pia yanadhoofisha ukusanyaji wa taarifa za kijasusi kwa kuwa yanaharibu uaminifu kati ya umma na polisi,” anaongeza.

Wakili huyo anaitaka mahakama itangaze kuwa maagizo hayo ni kinyume cha Katiba na kuzuia Inspekta Jenerali na maafisa walio chini yake kutekeleza maagizo hayo yaliyotolewa na Rais na Waziri.