Makala

Hofu yazima matumaini ya waathiriwa wa mafuta licha ya fidia nono

July 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Hadi majuma mawili yaliyopita, ambapo wakazi wa sehemu ya Makueni walishinda kesi ya uchafuzi wa mazingira dhidi ya Kampuni ya Bomba ya Mafuta Kenya (KPC) na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kuhusu kuvuja kwa mafuta mwaka 2015, mlalamishi mkuu, Muindi Kimeu, alikuwa akikejeliwa na baadhi ya majirani zake.

Walidai kuwa Kimeu, ambaye aliacha shule akiwa darasa la nane, hakuwa na uwezo wa kupambana na shirika la serikali.

Tangu uamuzi huo, Kimeu amekuwa kipenzi cha kijiji kizima cha Thange.

Wakazi wa Thange kwa makumi wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa Kimeu kila siku, wengine kuthibitisha maelezo yao na wengine kumsihi awaongeze kwenye orodha ya watu 3,075 wanaotarajiwa kupokea Sh2.1 bilioni.

Kiasi cha pesa ambacho kila mkazi atapokea kitategemea kiwango ambacho maisha yao yameathiriwa na kuvuja kwa mafuta, ikiwa ni pamoja na thibitisho la kupoteza mifugo, ukubwa wa ardhi iliyoathiriwa na gharama za matibabu walizolipa.

“Kwa sasa siwezi kufanya chochote,” Kimeu alimwambia mama mzee aliyedai kuwa afya yake ilidorora miaka ya hivi karibuni. Haikubainika mara moja ni kwa nini mkazi huyo wa Thange hakuwa miongoni mwa walalamishi 3,075. Kimeu alimshauri ajiunge na juhudi mpya za kushtaki KPC kuhusu kuvuja kwa mafuta, juhudi zinazoongozwa na Seneta wa Makueni, Daniel Maanzo.

“Mna kila sababu ya kushirikiana na kusherehekea kwa sababu Thange inatarajia kupokea pesa nyingi zaidi ya bajeti ya maendeleo ya serikali ya Kaunti ya Makueni kwa mwaka mzima,” alisema Mwakilishi wa Wadi ya Thange, Eric Katumo, alipokuwa akizungumza na makundi mawili ya wakazi waliokuwa wakizozana kuhusu nani ana haki ya kufaidika na mabilioni yaliyotolewa na Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Makueni kwa waathiriwa wa kuvuja kwa mafuta Thange.

Uamuzi wa mahakama uliofanywa Julai 11 ulitarajiwa kuleta mwanga wa matumaini katika kijiji cha Thange, ambacho kimekuwa kikihangaika na madhara ya mafuta kwa miaka kumi. Hata hivyo, mvutano kuhusu mgao wa fedha hizo umepunguza shangwe hiyo. Badala yake, kijiji kimezama katika hali ya kukata tamaa huku wakazi wake wakiteseka na magonjwa ya ajabu na hofu kwamba KPC na NEMA zitawasilisha rufaa kupinga uamuzi huo.

“Tunatarajia kupokea angalau Sh 900,000 katika siku 120 zijazo. Kwa bahati mbaya, hatutafurahia pesa hizo kwa sababu tumeathirika kiafya. Sehemu kubwa ya pesa hizo itaishia hospitalini,” alisema Mary Ndunge, mkulima mdogo wa kijiji cha Mwanza, ambaye aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa figo.

Kijijini Moki, mhudumu wa afya ya jamii ambaye pia ni miongoni mwa wakazi wengi wa Thange wanaougua magonjwa ya ini na figo, anatarajia kupokea angalau Sh1.5 milioni kutoka kwa mgao huo wa KPC. Alipoulizwa, alisema angefurahi zaidi iwapo mahakama ingekubali ombi la walalamishi kuanzishwa kwa hospitali ya kisasa eneo hilo ili kushughulikia matatizo ya kiafya yanayotokana na kuvuja kwa mafuta.

“Sehemu kubwa ya pesa nitakazopokea zitatumika kwa matibabu. Zilizobaki nitazitumia kununua upya mifugo niliopoteza kutokana na sumu ya mafuta,” alisema Paul Kalai alipoongea na Taifa leo.