Habari za Kitaifa

Maseneta wataka sheria ibadilishwe wakimezea mate majukumu ya wabunge

Na  MOSES NYAMORI July 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Maseneta wameanzisha juhudi mpya za kupanua mamlaka yao ya kisheria wapate nguvu za kuwahoji na kuidhinisha maafisa wakuu wa serikali kama Mawaziri na makatibu wa wizara.

Kupitia Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya wa mwaka 2025, Seneti inapendekeza mabadiliko ya Katiba ili kuanzisha Hazina ya Mabunge ya Kaunti itakayowezesha madiwani kutekeleza wajibu mkubwa zaidi wa usimamizi.

Mswada huo pia unapendekeza kupanua jukumu la Seneti katika mchakato wa kuandaa bajeti ya taifa, kwa kuhakikisha kuwa Mabunge yote mawili — Seneti na Bunge la Kitaifa — yanashiriki kwa usawa katika hatua hiyo muhimu.

Katika hatua ambayo huenda ikachochea uhasama uliopo kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa, Mswada huo unapendekeza kurekebisha vifungu vya Katiba: 157, 215, 228, 229, 233 na 250, ili kugawa jukumu la kuwahoji na kuwaidhinisha maafisa mbalimbali wa serikali kati ya mabunge yote mawili.

Kwa sasa, kazi ya kuwahoji na kuwaidhinisha maafisa wa serikali — wakiwemo Waziri, Katibu, Mabalozi na wengineo — ni jukumu la kipekee la Bunge la Kitaifa, isipokuwa kwa baadhi ya nafasi maalum kama vile Inspekta Jenerali wa Polisi na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, ambapo Seneti hushirikiana na Bunge la Kitaifa katika mchakato huo.

“Kulingana na marekebisho yaliyopendekezwa kwa Kifungu cha 250 cha Katiba, Mswada unapendekeza pia kurekebisha Kifungu cha 251 ili kuwezesha mabunge yote mawili kushiriki katika mchakato wa kumuondoa afisa wa tume au ofisi huru kutoka kazini,” unasema Mswada huo.

Mswada huo umeungwa mkono kwa pamoja na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na Kiongozi wa Wachache Stewart Madzayo.

Mswada huu pia unapendekeza marekebisho ya Kifungu cha 115 cha Katiba, ili kuifanya miswada yote iliyopitishwa na Bunge kuwasilishwa kwa pamoja na maspika wa mabunge yote kwa Rais ili kuidhinishwa.

Mswada unalenga kurekebisha Kifungu cha 109 ili kuruhusu mswada wowote kuanzishwa katika mojawapo ya mabunge hayo mawili, isipokuwa miswada ya ukusanyaji wa mapato ya kitaifa ambayo itasalia kuanzishwa katika Bunge la Kitaifa pekee.

Kwa sasa, mamlaka ya kuanzisha mchakato wa kumwondoa afisa wa tume au ofisi huru ni ya kipekee kwa Bunge la Kitaifa, lakini Mswada unapendekeza kugawa jukumu hilo kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa.