Hospitali zakataa wagonjwa bila hela SHA ikikazwa
Hospitali za rufaa kote nchini Kenya zimeanza kuwakataa wagonjwa wanaofika kutafuta matibabu bila pesa taslimu, sera inayowazuia mamilioni ya Wakenya katika sekta isiyo rasmi kupata huduma muhimu za afya.
Notisi ya ndani ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ya Julai 22, 2025, ambayo Taifa Leo imepata, inaonyesha jinsi hospitali za umma sasa zinahimiza malipo ya papo kwa papo kuwahudumia wagonjwa.
Notisi hiyo, iliyotiwa saini na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Dkt William Sigilai, na kutumwa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Magonjwa na Taarifa za Afya, inasema:”Kuanzia leo, wagonjwa wote wanaotaka kulazwa bila kuwa na bima halali ya afya watalazimika kulipa ada ya awali ya kulazwa au gharama ya upasuaji kabla ya kupokea huduma, isipokuwa tu ikiwa ni dharura.”
Agizo hilo linaeleza kuwa malipo hayo ya awali “yanahakikisha hospitali inaweza kugharamia huduma za mwanzo na kupunguza hatari ya bili kutolipwa,” na hivyo kuweka mbele usalama wa kifedha wa taasisi kuliko ustawi wa mgonjwa.
Sera hii inatekelezwa wakati ambapo mamilioni ya Wakenya wanaotegemea hospitali hizi hawana bima ya afya inayotumika. Kulingana na takwimu rasmi, ingawa zaidi ya Wakenya milioni 18.5 wamesajiliwa kwenye mpango wa bima ya serikali, ni milioni 3.5 pekee wanaotoka sekta rasmi.
Cha kusikitisha zaidi, kati ya Wakenya milioni 4.6 waliopimwa uwezo wao wa kuchangia, ni milioni 1.2 pekee waliowahi kulipa, huku wanaolipa kikamilifu wakiwa watu 500,000.
Muundo wa malipo ya kila mwaka unawaathiri zaidi wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi ambao ni asilimia 83 ya nguvu kazi nchini. Wengi wao hujipatia kipato cha kila mwezi kutokana na biashara ndogo ndogo, kilimo, na ajira za mikono. Hata hivyo, wanatatizika kulipa mara moja.
Awali, walikuwa wakilipa kati ya Sh500 hadi Sh1,000 kila mwezi. Sasa wanalazimika kulipa kati ya Sh6,000 hadi Sh12,000 mara moja kwa mwaka — jambo linalowatenga kwenye mfumo wa afya.
Katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga mjini Kisumu, utekelezaji wa sera hiyo ni wa moja kwa moja. Wagonjwa wasio na usajili kamili wa bima wanatakiwa kulipa pesa taslimu kabla ya kulazwa.
Maafisa wa hospitali hiyo wanasema huwa wanawaelekeza wagonjwa kujisajili kwa bima mara moja au wajiandae kulipa gharama kubwa kwa pesa taslimu.
“Bila bima, unalipa taslimu. Ukiwa na bima, unalipiwa kupitia mpango,” alisema msimamizi mmoja wa hospitali, akiongeza kuwa wagonjwa wanaojisajili wakati tayari wamelazwa watalazimika kulipa gharama kabla bima yao kuanza kazi.
“Ukilazwa kabla bima yako kuanza kutumika, utalipia kipindi hicho kwa pesa taslimu. Itakapoanza, bili zitachukuliwa na bima,” aliongeza.
Katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret, wagonjwa wasio na pesa wala bima hawakataliwi mara moja, lakini hupelekwa katika “wingi ya mkopo” hadi watakapoweza kulipa.
Hospitali zimekuwa zikilalamikia kucheleweshwa kwa malipo na madeni ya mamilioni kutoka kwa mpango wa bima ya serikali, hali inayozilazimisha kuanzisha sera kali za malipo ya taslimu ili kuendelea kutoa huduma.
Chama cha Hospitali za Kibinafsi za Mashinani (RUPHA) kimeripoti kuwa wanachama wake wanalazimika kukopa fedha benki ili kuendelea kutoa huduma huku wakisubiri malipo ya serikali.
Mgogoro huu umechochewa zaidi na kushindwa kwa sekta isiyo rasmi kushiriki ipasavyo kwenye bima ya afya, ambapo ni asilimia 10 tu ya waliopimwa uwezo wa kulipa waliochangia kikamilifu.