Korti yazuia magavana kupata hela za barabara wanazopigania na wabunge
Wabunge na Magavana wanavutana katika mzozo mpya wa kisheria katika Mahakama ya Rufaa kuhusu udhibiti wa mabilioni ya pesa zinazokusanywa na serikali chini ya Hazina ya Ukarabati wa Barabara (RMLF).
Mgogoro huu unahusiana na uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuagiza Sh10.5 bilioni zipatiwe kaunti kwa ukarabati wa barabara, hadi rufaa iliyowasilishwa na Bunge la Kitaifa na Bodi ya Barabara ya Kenya itakaposikilizwa.
Mahakama ya Rufaa Ijumaa ilizuia utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuruhusu walalamishi kufuatilia rufaa yao. Hii inazuia kaunti kupokea fedha hizo hadi Mahakama ya Rufaa itakapoamuru vinginevyo.
Uamuzi huo ulitolewa na Majaji Daniel Musinga, Pauline Nyamweya na George Odunga wakati ambao kaunti zilikuwa zikisubiri mgao wa Sh6.8 bilioni kati ya Sh10.5 bilioni ambazo Magavana walisema ni haki yao kwa ukarabati wa barabara katika mwaka wa fedha wa 2024/25.
Hati za mahakama zinaonyesha Sh3.6 bilioni tu ndizo zimetolewa hadi sasa.