Sheria:Lazima upate idhini ya mume au mkeo kabla ya kuuza mali ya ndoa
Idhini ya ya wanandoa wote wawili inahitajika kabla ya kuuza, kuhamisha, kupangisha, kuweka rehani au kutoa mali ya ndoa kwa namna yoyote ile.
Mali ya ndoa inamaanisha makazi ya ndoa, vifaa vya nyumbani na vitu vilivyomo ndani ya makazi ya ndoa au makazi mengine ya ndoa, pamoja na mali nyingine yoyote ya kudumu au isiyo ya kudumu ambayo inamilikiwa kwa pamoja na wanandoa na iliyonunuliwa wakati. Ni muhimu kufahamu kwamba mali inayoshikiliwa kwa misingi ya mila kama ya kurithi, haitambuliwi kama mali ya ndoa.
Isipokuwa wanandoa wakubaliane vinginevyo, umiliki wa mali ya ndoa unatokana na mchango wa kila mmoja katika ununuzi wake, na hugawanywa kati yao iwapo wataachana au ndoa yao kuvunjika.
Watu wanaokusudia kuoana wanaweza kukubaliana kabla ya ndoa yao kuhusu haki yao ya mali. Makubaliano haya yanaweza kufutwa na Mahakama ikiwa yatafanywa kwa udanganyifu, shinikizo au dhuluma dhahiri.
Wanandoa wana haki na wajibu sawa wakati wa ndoa, wakati ndoa ikiendelea na hata pale ndoa inapovunjwa. Hii ni kulingana na Ibara ya 45(3) ya Katiba na Kifungu cha 4 cha Sheria ya Mali ya Ndoa.
Endapo mmoja wa wanandoa atachangia kuboresha mali yoyote, iwe ilinunuliwa kabla au wakati wa ndoa, lakini mali hiyo haikupatikana wakati wa ndoa, basi hupata maslahi ya manufaa katika mali hiyo kulingana na mchango wake.
Katika ndoa ya wake wengi, haki ya mali ya ndoa inayohusu mali iliyopatikana na mume na mke wa kwanza humilikiwa kwa usawa kati yao wawili, ikiwa mali hiyo ilipatikana kabla ya mume kuoa wake wengine.
Iwapo mali ya ndoa ilipatikana baada ya mume kuoa mke mwingine, basi haki ya mali hugawanywa kati ya mume na wake wote, kwa kuzingatia mchango wa kila mmoja.
Hata hivyo, ikiwa kuna makubaliano kwamba mke atamiliki mali ya ndoa na mume wake pekee, basi mke huyo humiliki mali hiyo kwa usawa na mume wake bila kuhusisha wake wengine.
Deni lolote linalochukuliwa na mmoja wa wanandoa kabla ya ndoa litasalia kuwa jukumu la mume au mke huyo hata baada ya ndoa. Iwapo mali hiyo itakuwa mali ya ndoa, basi deni hilo litagawanywa sawa isipokuwa kuwe na makubaliano tofauti.
Deni lolote linalopatikana wakati ndoa ikiendelea au gharama yoyote halali kwa faida ya ndoa, hugawanywa sawa kati ya wanandoa.
Katika ugavi wa mali ya ndoa, sheria za kimila za jamii husika zitazingatiwa, lakini lazima ziambatane na maadili na misingi ya Katiba.