Makundi ya kutetea haki yashinikiza kuachiliwa mwanaharakati Mwagodi
MAKUNDI ya kutetea haki za kibinadamu sasa yanashinikiza kuachiliwa huru kwa mwanaharakati Mwabili Mwagodi, aliyedaiwa kutekwa nyara nchini Tanzania Jumatano.
Jana, Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC), shirika la Vocal Africa na lile la Amnesty International zilitoa taarifa zikiitaka serikali ya Tanzania imwachilie huru mwanaharakati huyo ambaye amekuwa akifanya kazi katika mkahawa mmoja jijini Dar es Salam.
KHRC ilielezea hofu kwamba hakuna afisa wa serikali za Tanzania na Kenya aliyejitokeza kuelezea aliko Bw Mwagodi.
“Familia yake inathibitisha kuwa Mwagodi alikuwa akichunguzwa na maafisa wa usalama wa Kenya baada ya yeye kutekeleza haki yake ya kushiriki maandamano. Mwagodi aliongoza maandamano dhidi ya utawala wa Rais William Ruto wakati wa ibada katika kanisa moja mjini Nyahururu, kaunti ya Laikipia,” taarifa hiyo ikaeleza.
Kulingana na KHRC Kenya inashirikiana na Tanzania kimakusudi katika matumizi ya nguvu dhalimu kupamba na wanaharakati kwa namna iliyopangwa.
“Mienendo hii inaashiria kuwa tawala za kiimla za Kenya na Tanzania zimepoteza haki ya kuongoza. Hatujasahau kuwa miezi miwili iliyopita, Kenya ilishirikiana katika utekaji nyara na kuteswa kwa mwanaharakati Boniface Mwangi na maafisa wa usalama wa Tanzania,” tume hiyo ikaeleza.
Kwa hivyo, KHRC sasa imewasilisha matakwa kadhaa ikiwemo kuachiliwa huru kwa Bw Mwagodi anayezuiliwa kinyume cha sheria nchini Tanzania.Aidha, mashirika hayo yanazitaka serikali za Tanzania na Kenya zieleze aliko mwanaharakati huyo na familia na mawakili wake waruhusiwe kumfikia.
Vile vile, yanataka uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu vitisho vilivyotolewa kwa familia ya Mwagodi na maafisa wa usalama wa Kenya.
Kwingineko, Shirika la Amnesty International pia limelalamika kuhusu ripoti za kutekwa nyara na kutoweka kwa Bw Mwagodi.
Mkurugenzi wa shirika hilo Houghton Irungu, kwenye taarifa alisema uanaharakati sio hatia na kwamba anapaswa kuachiliwa huru mara moja.
“Uanaharakati wa Mwabili Mwagodi sio kitendo cha uhalifu. Lakini kutoweka kwake ni hatia, ni ukiukaji wa haki za kibinadamu na unapasa kushughulikiwa kwa dhararu na kwa uwajibikaji,” Bw Irungu akasema.