Tawi la hospitali lafungwa kufuatia kuuawa kwa mgonjwa aliyelazwa
BARAZA la Madaktari Nchini Kenya (KMPDC) limeamuru kuhamishwa mara moja kwa wagonjwa wote kutoka Tawi la Braeside la Chiromo Hospital Group lililoko Lavington.
Hili limejiri kufuatia kifo cha kutatanisha cha Susan Kamengere Njoki, muuguzi na mkurugenzi mkuu wa shirika la Toto Touch, ambaye alithibitishwa kuuawa wakati alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali hiyo inayomilikiwa na Chiromo Group of Hospitals.
Ripoti ya upasuaji wa maiti ilionyesha kuwa Bi Njoki alifariki kutokana na majeraha yaliyotokana na kunyongwa kwa mikono.
Ripoti hiyo pia iligundua dalili nyingine za kitabibu ambazo hazihusiani moja kwa moja na chanzo cha kifo, lakini huenda zilihusiana na hali nyingine aliyokuwa akitibiwa wakati wa kulazwa hospitalini.
Katika barua iliyoandikwa Julai 25, 2025, iliyowasilishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, baraza hilo liliamuru hospitali hiyo kusitisha huduma zote za matabibu mara moja na kuhamisha wagonjwa wote ndani ya saa 24 tangu kupokea taarifa hiyo.
“Baada ya ripoti zaidi kuashiria uwezekano wa kuhusika kwa mfanyakazi mmoja wa hospitali yenu katika kifo cha Bi Susan Kamengere Njoki, Baraza linatoa maagizo yafuatayo yanayotekelezwa mara moja: Mhamishe wagonjwa wote ndani ya saa ishirini na nne (24) tangu kupokea barua hii. Simamisha huduma zote za matabibu katika Tawi la Chiromo Braeside hadi itakapotangazwa vinginevyo,” ilisema barua iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu Dkt David G. Kariuki.
Baraza hilo lilitaja sababu za usalama wa umma na likatumia Kanuni ya 8 ya Sheria Ndogo za Madaktari na Madaktari wa Meno (Uchunguzi na Nidhamu) za mwaka 2022, chini ya Sura ya 253 ya Sheria za Kenya.
“Maagizo haya yametolewa chini ya Sheria Ndogo za Madaktari na Madaktari wa Meno (Uchunguzi na Nidhamu) za mwaka 2022, Kanuni ya 8, kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa wagonjwa na kurejesha imani ya umma katika mfumo wa afya,” alisema Dkt Kariuki.
“Baraza linaendelea kujitolea kuhakikisha usalama wa wagonjwa na kudumisha viwango vya juu vya huduma ya afya,” aliongeza.
Mbali na kufunga hospitali hiyo, KMPDC imeitaka Chiromo Group kutoa majibu ya haraka kwa barua hiyo, ikijumuisha ripoti ya upasuaji wa maiti, rekodi za wagonjwa na stakabadhi nyingine muhimu kwa uchunguzi unaoendelea.
Hospitali hiyo pia imeagizwa kuwasilisha ripoti ya kina ikieleza hatua za tahadhari zilizochukuliwa ili kuzuia matukio kama hayo siku zijazo.
“Mnaagizwa kuwasilisha nakala za ripoti ya upasuaji wa maiti, rekodi zote muhimu za wagonjwa na stakabadhi zinazohitajika, na kutoa ripoti kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kuzuia matukio kama hayo baadaye,” alisema Dkt Kariuki.
Kupitia mitandao ya kijamii, KMPDC ilitangaza kuwa imeanzisha uchunguzi kuhusu mazingira ya kifo cha Susan Njoki.