Habari za Kitaifa

Tanzania yaachilia mwanaharakati wa Kenya Mwabili Mwagodi baada ya presha

Na CHARLES WASONGA July 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAHARAKATI Mwabili Mwagodi, aliyeripotiwa kutoweka jijini Dar es Salaam, Tanzania, Jumatano, amepatikana akiwa hai.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu Jumapili asubuhi yalithibitisha kuwa Mwagodi alipatikana akiwa ametelekezwa msituni katika eneo la Kinondo, karibu na Diani, kaunti ya Kwale.

“Mwabili Mwagodi amepatikana akiwa hai baada ya kutoweka Tanzania. Tunashukuru presha iliyowekwa na familia ya Mwabili, umma na makundi ya kutetea haki. Kila mtu aliyepaza sauti yake amewezesha hili kufanyika. Lakini unyamavu wa maafisa wa serikali za Tanzania na Kenya ungali unachukiza,” shirika la Vocal Afrika likasema kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa X (zamani twitter).

“Tunaendelea kushinikiza kuwa uchunguzi huru ufanyike, uwajibikaji mbele ya Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu Haki na ulinzi kwa Mwabili na wanaharakati wengine wanaokabiliwa na haki ya kukamatwa,” shirika hilo likaongeza.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Vocal Afrika Hussein Khalid alisema Mwabili alikimbizwa katika Hospitali ya Pandya, Mombasa kufanyiwa ukaguzi wa kiafya.

“Wakati huu, Mwabili amekimbizwa katia Hospitali ya Pandya, Mombasa kwa ukaguzi wa dharura na baadaye atasafirishwa kwa ndege hadi Nairobi kuungana na familia yake,” akaeleza.

Mwabili, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Kenya Kwanza aliripotiwa kukamatwa na maafisa wa usalama Jumatano akiwa njiani akielekea hoteli moja eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, anakofanyia kazi.

Familia ilidai kuwa mienendo yake imekuwa ikichunguzwa na serikali ya Kenya kutokana na kuhusika kwake na maandamano ya vijana wa Gen Z, Juni 2024.

Mnamo Jumamosi makundi ya kutetea haki yalishinikiza kuachiliwa kwa Mwabili.

Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC), Vocal Africa na lile la Amnesty International zilitoa taarifa zikiitaka serikali ya Tanzania imwachilie huru mwanaharakati huyo ambaye amekuwa akifanyakazi katika mkahawa mmoja jijini Dar es Salam.

KHRC ilielezea hofu kwamba hamna afisa wa serikali za Tanzania na Kenya wamejitokeza kuelezea aliko Bw Mwagodi.

“Familia yake inathibitisha kuwa Mwagodi alikuwa akichunguzwa na maafisa wa usalama wa Kenya baada ya yeye kutekeleza haki yake ya kushiriki maandamano. Mwagodi aliongoza maandamano dhidi ya utawala wa Rais William Ruto wakati wa ibada katika kanisa moja mjini Nyahururu, kaunti ya Laikipia,” taarifa hiyo ikaeleza.