Habari

Mkosoaji wa Ruto alivyopatwa ametupwa mpakani Lunga Lunga hajijui hajitambui

Na KEVIN MUTAI July 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAHARAKATI wa Haki za Kibinadamu Mwabili Mwagodi ambaye alitoweka Tanzania Jumapili, Julai 27, 2025 alikuwa akitarajiwa kuhamishwa Nairobi japo bado alikuwa akiendelea kupokea matibabu kwenye hospitali moja Mombasa baada ya kupatikana ametelekezwa Kaunti ya Kwale.

Waliompeleka hospitalini walisema alipatikana hajijui hajitambui Lunga Lunga na watu ambao wanaaminika kuwa polisi waliovalia nguo za kiraia.

Lunga Lunga ipo kwenye mpaka wa Kenya-Tanzania umbali wa kilomita 60 kutoka Kinondo.

Kwa mujibu wa afisa wa Wanaharakati wa Waislamu (MUHURI) Francis Auma, alipatikana saa tisa asubuhi ya kuamkia Jumapili kisha akasafirishwa Mombasa.

“Hii sasa ni kama imezoeleka. Tulikiona kile kilichofanyikia Boniface Mwangi ambaye alitekwa nyara Tanzania kisha akatelekezwa kwenye mpaka,” akasema Bw Auma.

Mjomba wa Bw Mwagodi Zacharia Mwabili ambaye alikuwa na wanafamilia wengine alisema mwanafamilia wao alikuwa akihisi uchungu na alihitaji matibabu ya dharura.

“Ni kutokana na miujiza ya Mwenyezi Mungu kuwa tumempata. Tulikuwa tumeingiwa sana na wasiwasi kuhusu maisha yake,” akasema Bw Zacharia.

Familia yake ilisema kuwa Bw Mwagodi alikuwa amewafichulia alihojiwa na makachero kutoka Tanzana.

Makachero hao walitaka kujua nia yake ya kutembelea taifa hilo na iwapo alikuwa na uhusiano wowote wa kisiasa huko.

Mwanaharakati huyo amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Rais William Ruto na ni kati ya wanaharakati ambao wamekuwa wakiongoza maandamano dhidi ya serikali.

Alikuwa mstari wa mbele wakati wa maandamano ya 2024 ya kupinga Mswada wa Fedha na alikuwa akiwaongoza wenyeji wa Pwani kushiriki maandamano hayo.

“Walichukua stakabadhi zake ikiwemo zile za kusafiri, simu pesa na hata kitambulisho chake,” akasema Bw Zacharia.

Wanaharakati waliomchukua kutoka Diani walifichua kuwa alikuwa ameteswa na kufichwa kwenye chumba chenye giza tororo alikotengwa.

Pia walishutumu polisi wakisema walimtishia Bw Mwagodi akiwa hospitalini na wakawataka wale ambao walikuwa wamefika hospitalibni wampe muda apate nafuu kabla ya kumhoji.

“Walimtesa na unaona hayuko vyema kiakili. Amesema walimpiga kisha kumdunga kwa kitu asichofahamu ndiposa tunataka atibiwe haraka iwezekanavyo,” akasema Mwanaharakati Walid Said.

Kutekwa nyara kwake Jumatano wiki jana kulikuwa kumezua vurumai mitandaoni huku wengi wakitaka aachiliwe huru.

Makundi ya haki sasa yanaitaka serikali ichukue hatua dhidi ya waliomteka nyara.