Murkomen: Kama wewe ni jangili na una bunduki, isalimishe; tutakusomesha na tukupe ajira
WAZIRI wa Usalama Kipchumba Murkomen amesema serikali sasa itaelimisha na kuwapiga jeki kwa kuwapa ajira majangili ambao watawasilisha bundiki zao na kuasi uhalifu Kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Kwa zaidi ya miaka 40 wanajeshi, vikosi mbalimbali vya polisi wamekuwa wakipambana na ujangili Baringo, Samburu, Elgeyo Maraket, Pokot Magharibi na Laikipia.
“Serikali inawaomba wale majangili wenye bunduki wazisalimishe. Ukifanya hivyo, tutakusomesha kwenye taasisi za masomo, vyuo vya kiufundi na taasisi nyingine za masomo,” akasema Bw Murkomen.
“Tutawapa majangili ufadhili na wakifuzu, tutawapa ajira kwenye miradi ya serikali kama ile ya kujenga nyumba za gharama nafuu na kwenye mashirika mengine ya serikali,” akaongeza.
Alikuwa akiongea wakati wa Kongamano la Jukwaa la Usalama kwenye kaunti za Kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Aliwataka majangili hao wahakikishe kuwa wanawasilisha bunduki zao zote badala ya kusubiri kukabiliwa na maafisa wa usalama.
Alisema serikali ina mpango wa kukabiliana na majangili wanaosababisha utovu wa usalama ukanda huo kuhakikisha amani inapatikana.
“Vijana majangili ni wale ambao wamefika umri wa kuenda shule gili na wakibadilika, tutawasaidia kuwa na maisha mazuri. Wale ambao wataendeleza ujangili, hawatakuwa na wa kumlaumu tukiwakabili,” akaongeza.
Bw Murkomen alifichua kuwa tangu serikali ianze oparesheni, bunduki 1,000 zimetwaliwa na juhudi zinaendelea kutwaa nyingine 10,000 ambazo bado zipo mikononi mwa majangili.
Kauli ya Murkomen inakuja wakati baadhi ya viongoiz nwa kaunti za Baringo na Samburu wameitaka serikali itenge Sh20 bilioni kufungua kaunti za Kaskazini Mashariki.