Habari za Kitaifa

Wanafanya kama Azimio? Upinzani waanza kugawa mamlaka hata kabla ya 2027

Na JUSTUS OCHIENG’ July 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amefichua kuwa upinzani umeanza kufanyia kazi mkataba wa kugawa mamlaka kuhakikisha wanamshinda Rais William Ruto mnamo 2027.

Duru kutoka muungano huo ziliarifu kuwa kumeibuka stakabadhi tano za kugawana mamlaka ambazo zimeanza kujadiliwa.

Akiongea akiwa Amerika ambako yuko kwa ziara ya mwezi moja, Bw Gachagua alisema serikali ni kubwa na ina nafasi ya kila mtu.

“Tutakubaliana nani anachukua wadhifa upi mradi tu tuna fomyula ya uongozi mzuri ambao utamaliza ufisadi, mauaji na utekaji nyara. Hilo ni suala ambalo halihitaji mjadala au ufafanuzi,” akasema Bw Gachagua baada ya kuandaa mazungumzo na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí Amerika mnamo Jumamosi.

Kando na Bw Gachagua, vigogo wengine wa upinzani ni Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa PLP Martha Karua na Eugene Wamalwa wa DAP-K pamoja na Justin Muturi wa DP.

Taifa Leo imebaini kuwa kamati ya kiufundi ya upinzani imeibuka na stakabadhi tano za kugawana mamlaka.

Kati ya nafasi ambazo zinaangizwa sana ni Rais, Naibu Rais na Waziri Mkuu pamoja na Maspika wa Seneti na Bunge la Kitaifa.

Japo wadhifa wa waziri mkuu haupo kwenye katiba, kamati ya kiufundi inapendekeza marekebisho ya katiba ili iwekwe baada ya uchaguzi wa 2027.

Mnamo 2022, Rais Ruto alibuni wadhifa wa Kinara wa Mawaziri ambao sasa unashikiliwa na Musalia Mudavadi kama sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa kugawa mamlaka ndani ya Kenya Kwanza.

Katika pendekezo la kwanza Bw Musyoka anapigiwa upato kama mwaniaji wa urais huku Bw Wamalwa, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na Dkt Fred Matiangí wakitajwa kuwa mmoja wao atakuwa mgombeaji mwenza wake.  Bw Gachagua ametengewa wadhifa wa waziri mkuu.

Pendekezo la pili ni Bw Matiang’i awanie urais kisha mmoja kati ya Bw Musyoka, Bw Muturi na Bi Karua  awe mgombeaji mwenza wake. Pia hapa Bw Gachagua bado atakuwa waziri mkuu pamoja na Mabw Natembeya na Wamalwa.

Katika pendekezo la tatu, Bw Gachagua atakuwa mpeperushaji bendera wa upinzani lakini hilo litategemea uamuzi wa kesi iliyo kortini kufuatia kutimuliwa kwake mnamo Oktoba 2024 kama Naibu Rais.

 Bw Wamalwa, Dkt Matiangí au Bw Natembeya hapa wametajwa kama mgombeaji mwenza kisha Bw Musyoka akiwa waziri mkuu.

Vilevile upinzani unapendekeza Bi Karua awe mwaniaji wao kisha Mabw Matiang’i, Wamalwa, au Natembeya mmoja kati yao awe mgombeaji mwenza.  Bw Musyoka anapendekezwa kuwa waziri mkuu.

Pendekezo la mwisho linamweka Bw Wamalwa kama mwaniaji wa urais kisha Mabw Musyoka, Muturi pamoja na Bi Karua kama mgombeaji mwenza. Bw Gachagua au Dkt Matiangí atakuwa waziri mkuu.

Uamuzi wa mwisho kuhusu mapendekezo hayo utafanywa na vinara wenyewe kisha watie saini makubaliano ya kuidhinisha pendekezo ambalo litakumbatiwa.