Habari

Askofu aliyeonekana kumponda Gachagua na Matiang’i abadili mawazo baada ya kukosolewa

Na WYCLIFFE NYABERI July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ASKOFU wa Kanisa Katoliki dayosisi ya Kisii Joseph Mairura Okemwa ameonekana kubadilisha mawazo yake kuhusu upinzani baada ya kukosolewa mtandaoni.

Alipokuwa akiwaongoza waumini wa Kanisa Katoliki katika misa ya shukrani katika Shule ya Upili ya Cardinal Otunga Mosocho wiki moja iliyopita, Askofu Mairura aliwakashifu viongozi wa upinzani ambao hakuwataja kwa ziara zao katika nchi ya Amerika.

Kasisi huyo ambaye alikuwa akisherehekea kuhitimu miaka 70 na kuhudumia kanisa kwa zaidi ya miaka 30 alionekana kumtetea Rais William Ruto na Utawala wake wa Kenya Kwanza huku akikemea vikali upinzani.

“Wakristo wenzangu, niwaulize, tuna rais nchini Kenya? Yuko ama hayuko? Si yuko? Huyo ndiye mliyempigia kura na tunamtambua. Kama humtambui, nenda Amerika, lakini msiseme ni sisi tuliowatuma. Ni nani aliyetuma watu kwenda kuzungumza Amerika?” Askofu Mairura aliuliza.

Baadhi ya Wakenya waliokerwa na kasisi huyo walianza kumzomea, wakimlaumu kwa kuegemea upande wa baadhi ya wanasiasa.

Wengine walidai amechagua kumsifu Rais William Ruto ili aendelee kupokea heri zaidi kutoka kwake.

Kufuatia mashambulizi ya wiki moja dhidi yake, Askofu Mairura Jumapili alijitokeza na kusimulia jinsi alivyotaniwa na kudhalilishwa hadharani kwa kusema mawazo yake.

Akizungumza akiwaongoza waumini katika ibada ya kutakasa kanisa jipya la Nyamache, Askofu Mairura alisema alikosa usingizi kwa siku tatu kwa kejeli alizopewa mitandaoni.

“Kama mnavyoona sitembei vizuri. Sina nguvu kwa sababu nilivunjwa na kusagwa sagwa mitandaoni. Nimeona niwaambie. Tangu nilipozungumza mwisho, nimekaa siku tatu bila kulala kwa sababu ya watu nisiowafahamu walionidhalalisha na kunitukana sana.

“Nilijaribu kuwapuuza lakini ilikuwa vigumu na nilijiweka kwenye kikao na kuuliza ni nini hasa kinatokea. Jambo hili ni baya sana. Sikuwa na nia ya kumuudhi mtu yeyote nilipozungumza kuhusu watu kwenda Amerika. Wako huru. Lakini nilichosema kilionekana kuwa kimetolewa nje ya muktadha na kulikuwa na kutoelewana. Sikuwadhalalisha wana wetu huko Amerika,” Askofu Mairura alisema na kisha akawasihi wakosoaji hao kuachana.