Habari za Kitaifa

Familia za kifalme zaning’inia pabaya ushawishi ukiyumbishwa na ‘wadosi wapya’ wa siasa

Na JUSTUS OCHIENG’ July 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

HUKU familia ya rais wa pili nchini Daniel arap Moi ikiwa imepoteza ushawishi wake wa kisiasa na kimamlaka, familia za Kenyatta na Odinga zimekumbwa na wasiwasi katika mazingira ya sasa ya kisiasa.

Kwa sasa Rais William Ruto anashikilia mamlaka makuu nchini naye aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka wanashikilia usukani wa upinzani.

Wadadisi wanasema familia za Kenyatta na Odinga hazijizatiti tu kudumisha mamlaka na ushawishi unaozidi kuziteleza, bali mustakabali wazo katika ulingo wa siasa na uchumi.

“Familia kama hizi zinataka kusalia katika siasa si kwa ajili ya kutoa huduma au kuleta mageuzi, bali kwa sababu ya kumbukumbu za kisiasa na ushawishi. Hii ndiyo maana Sheria ya Vyama vya Kisiasa inapaswa kufanyiwa mabadiliko ili kuweka muda wa mtu kushikilia nafasi ya kiongozi wa chama cha kisiasa kuwa miaka minane au 10,” anasema Bw Javas Bigambo.

Anaongeza: “Mamlaka ya kisiasa huja na ushawishi mkubwa na manufaa ya kibiashara. Kile tunachoshuhudia ni msukumo wa kulinda utajiri na kukinga biashara zao zisichunguzwe.”

Kwa upande wake, Bw Martin Oloo, ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema, “Katika bara la Afrika, siasa huchukuliwa kama chombo cha kufanikisha uchumaji wa mali, sio huduma. Ni funzo linalotokana na ukoloni.”

“Familia za Odinga na Kenyatta zimefahamu mtindo huo wa kikoloni — wa kutumia mamlaka ya kisiasa si tu kujipa mali bali kulinda mali yao ya zamani.”

“Urais wa Uhuru (Kenyatta) ulipanua pakubwa mawanda ya kiuchumi ya familia yake, huku majaribio kadhaa ya Raila kuwania urais na handisheki yakiimarisha familia yake kiuchumi kwa kisingizio cha kupigania masilahi ya raia.”

Familia ya rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki pia inamulikwa baada ya kifo chake, huku mwanawe Jimmy Kibaki akishindwa kung’aa katika ulingo wa siasa.

Mnamo Mei 2024, Jimmy aliyeonekana kama mrithi wa kisiasa wa babake, alijiuzulu wadhifa wa naibu kiongoz wa chama cha The New Democrats (TND).

Lakini miezi michache baadaye, mnamo Septemba mwaka huo, alirejea tena na akaidhinishwa kama naibu kiongozi wa chama hicho hicho, kupitia tangazo lililowekwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa kwenye gazeti rasmi la serikali.

“Inaonekana kuwa watu hawa hawataki niende. Niliwaandikia barua ya kujiuzulu mwaka jana. Niliwasilisha nakala ya barua hiyo kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa. Nitafanya hivyo sasa,” Jimmy akaambia Taifa Leo, kupitia ujumbe mfupi, Jumanne.

Katibu Mkuu wa chama cha TND Daniel Musembi alisema wanavyofahamu, “Bado tunamtambua Jimmy kama afisa na mwanachama wetu.”

Prof Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multi-Media anasema “mamlaka ya kisiasa nchini Kenya hutumika kama kinga ya kulinda mamlaka ya familia za viongozi.”

“Kujiondoa kATIKA siasa ni sawa na kujiondolea kinga ya usalama.”

“Hizi familia za viongozi wa kisiasa haziendelei kujikaza katika siasa kwa sababu zina mamlaka – zinajikaza kwa sababu umma hauoni watakaochukua nafasi zao,” Prof Naituli anaongeza akielezea sababu zinazochangia familia za wanasiasa wakuu kutaka kuendelea kusalia katika ulingo wa siasa.

“Ikiwa hali hii haitabadilika, Kenya inakumbwa na hatari ya kutekwa katika hali ya kuendelea kuzifuata familia za wanasiasa wakuu kwa kisingizio kwamba zinawasaidia kupigania demokrasia.

Japo Rais Daniel arap Moi, alipokufa Februari 2020, aliacha familia iliyojikita katika siasa na biashara, hali ni tofauti sasa.

Ukosefu wa udhibiti wake umechangia kutokea kwa migawanyiko katika familia hiyo.

Jaribio la wanawe, Gideon na Raymond kuendelea kubeba mwenge wa kisiasa wa familia hiyo lilizimwa baada ya wawili hao kushindwa.

Gideon alipokonywa wadhifa wa useneta wa Baringo katika uchaguzi mkuu wa 2022 huku Raymond aking’atuliwa katika kiti chake cha ubunge wa Rongai na limbukeni Paul Chebor, aliyewania kwa tiketi ya chama cha UDA, chake Rais Ruto.

Bw Uhuru, mwanawe Rais wa kwanza nchini Jomo Kenyatta, pia anaendelea kupoteza ushawishi wa kisiasa baada ya kushindwa kwa chaguo lake katika uchaguzi mkuu wa 2022- – Bw Odinga.

Wandani wa Uhuru waliokuwa wakishikilia nyadhifa kubwa katika asasi za serikali wametimuliwa, biashara za familia ya Kenyatta nazo zimepigwa msasa.

Ushawishi wa Bw Uhuru katika ngome yake ya zamani ya Mlima Kenya, unaisha huku wakazi wakionekana kumkumbatia Gachagua.

Kwa upande wake, Bw Odinga anaonekana kuendeleza ushawishi wake katika ulingo wa siasa, kwa kusalia kiongozi wa ODM, baada ya kushindwa na Rais Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Japo Bw Odinga, aliyetimu umri wa miaka 80 alikuwa amewania kiti hicho mara nne na kushindwa, kushindwa kwake na Dkt Ruto kulikuwa pigo kubwa ikizingatiwa kuwa aliungwa mkono na Bw Uhuru na vyombo vyote vya dola.