Habari za Kitaifa

Murkomen: Kuna watu 161,000 Baringo hawajachukua vitambulisho, lazima tuwatafute

Na FLORAH KOECH July 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ZAIDI ya watu 161,000 katika kaunti ya Baringo hawana vitambulisho vya kitaifa, stakabadhi muhimu ya kuwawezesha kupata huduma za serikali na huduma nyinginezo.

Kulingana na Waziri wa Usalama, Bw Kipchumba Murkomen, eneo bunge la Tiaty ndilo lililoathirika zaidi kwani jumla ya watu 45,000 hawana vitambulisho vya kitaifa.

“Inasikitisha kuwa zaidi ya watu 161,000 katika kaunti ya Baringo hawana vitambulisho vya kitaifa. Hali hii inawafanya kukosa huduma muhimu na hata nafasi za ajira,” akasema Waziri Murkomen katika kikao cha Jukwaa la Usalama katika Chuo cha Mafunzo Anuai cha Baringo.

“Ajabu ni kwamba hata wazee wenye umri wa miaka 70 katika Tiaty hawana vitambulisho vya kitaifa, huu ni ubaguzi mkubwa. Labda hawaoni haja ya kuwa na vitambulisho kwa sababu huwa hawapati huduma za serikali,” akasema Waziri Murkomen katika kikao hicho kilichowaleta pamoja wakazi, viongozi, machifu na wakuu wa usalama.

Ukosefu wa vitambulisho pia umewazuia watoto kupata vyeti vya kuzaliwa, akasema Waziri huku akiahidi kuwa serikali inapanga kuanzisha mpango wa utoaji vitambulisho bila malipo kwa wakazi wa eneo la Tiaty.

“Aidha, tunapanga kuanzisha mfumo wa matumizi ya teknolojia katika utoaji vitambulisho kitaifa. Kupitia mfumo huo, waliotuma maomba wataweza kupata vitambulisho vyao ndani ya wiki tatu,” akaeleza.

Wakazi waliohojiwa walitaja utovu wa usalama kama kikwazo cha wao kutoweza kutuma maombi ya vitambulisho wakihojia kuandamwa na maafisa wa usalama.